RAIS
wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj
Dk. Hussein Ali Mwinyi, amejumuika na Waumini wa dini ya Kiislamu katika ibada ya
sala ya Ijumaa Msikiti wa Maungani, Wilaya ya Magharibi B.
Akitoa salamu kwa Waumini, Alhaj Dk. Mwinyi amewanasihi Vijana
kuwathamini wazazi wao na kuwatendea mema ili kupata baraka za Mwenyezi Mungu.
Alhaj Dk. Mwinyi amefahamisha ni wajibu na ni jambo jema
kwa vijana ambao wazazi wao wako hai kuishi nao kwa huruma na upendo na
kuwaombea dua wale waliotangulia mbele ya haki kwani kuna fadhila nyingi kwa
kutekeleza jambo hilo.
Akitoa hotuba ya Ijumaa Khatibu wa Msikiti wa Ijumaa wa
Maungani, Sheikh Suleiman Mwinchumu Suleiman amewasisitiza Waumini hao kuwa
karibu na wazazi wao pamoja na kuzungumza nao kwa maneno mazuri na kuacha
hasira juu yao kama ilivyoamrishwa na miongozo ya dini ya kiislamu.
Katibu Mtendaji wa Afisi ya Mufti, Sheikh Khalid Ali
Mfaume amesema ni vyema kwa Waumini wa kiislamu kufahamu du'a ya kuwaombea
wazee na kuitekeleza kila wanapopata fursa ya kufanya hivyo, Ili kupata radhi
za Mwenyezi Mungu.
Wakati huohuo, Alhaj Dk. Mwinyi baada ya sala ya Ijumaa
aliendeleza utaratibu wake wa kuwatembelea Wananchi na kuwajulia hali
Wagonjwa katika maeneo mbalimbali.
Aliowatembelea leo ni aliekuwa Mbunge na Naibu Waziri Mstaafu wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mshauri wa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wa Awamu ya Saba, Dk. Maua Abeid Daftari
anaeishi Beit Ras Wilaya ya Magharibi A.
Msanii Mkongwe wa sanaa za Filamu na Maigizo Zanzibar Bibi
Mwanamwema Khamis Juma, maarufu Bi Njiwa.
Mwengine ni Bi. Halima Muhamed, Mjane wa aliekuwa
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Kichama, Marehemu Borafya Silima wanaoishi
Mwera Mtofaani.
IDARA
YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment