Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kwamba serikali italifanyia kazi suala la
malalamiko ya wafanyabiashara wa masoko mbali mbali nchini kutolipwa fedha zao
na wenye mahoteli ambao wanachukua bidhaa zao bila kuwalipa kwa muda mrefu.
Mhe. Othman ameyasema hayo ofisini
kwake Migombani mjini Zanzibar,
alipokutana na uongozi wa Shirikisho la Umoja wa wafanyabiashara wa
Masokoni Zanzibar (SHIMAZA), kujitambulisha na azma yao ya kuendeleza shughuli
mbali mbali ikiwemo mashindano ya michezo na usafi wa mazingira kwa maendeleo
ya kibiashara kwa wajasiriamali hao.
Hata hivyo, pamoja na mambo mengine walilalamikia pia kukosa malipo ya bidhaa zao
zinazotumiwa na baadhi ya wenye mahoteli kwa muda mrefu na kuiomba serikali
isaidie uwezekano wa kupata malipo yao ili kuendeleza kazi zao za biashara
kwenye masoko hayo.
Mhe. Othman amesema kwamba serikali
inatambua kuwepo kadhia hiyo, kwa vile suala hilo liliwahi kujitokeza mwaka
2012 kwa uongozi wa iliyokuwa hoteli ya Venta Club kushindwa kuwalipa
wafanyabiashara wa masoko kwa bidhaa za mboga mboga na matunda walizozitumia.
Amefahamisha kwamba kutokana na
kujitokeza hali hiyo Serikali kupitia
Mamlaka ya Ukuzaji na Uendelezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) iliweka
utaratibu na mfumo maalumu wa kudibiti
hali hiyo isijitokeze tena lakini sasa
imejirejea.
Amesema kwamba jitiada zilizofanywa
na serikali wakati huo wa mwaka 2012 ilisaidia wafanyabiashara kulipwa fedha
zao na kuwekwa msisitizo wa kufuatwa utaratibu na Muongozo wa serikali chini ya
usimamizi wa ZIPA .
Hata hivyo, amewataka wafanyabiashara
hao kuondokana na dhana kwamba katika
masoko kuwa ni paala pa kuendeleza kazi
za kibiashara pekee , bali wazingatie
kwamba ni sehemu na hospitali ya mwanzo katika kulinda afya ya mwanadamu kwa
chakula anachotumia.
Amefaamisha wafanyabiashara wanapaswa
kuzingatia usafi wa hali ya juu kwenye bidhaa zao na kuachana na utamaduni wa mazoea wa kuuza bidhaa kwa
kuweka chini pamoja na mazingira yasioridhisha
jambo linaloweza kuhatarisha afya ya mtumiaji na pia kuzishusha thamani
bidhaa zao hasa kwa watumiaji wanaotoka nje ya Zanzibar.
Aidha amegusia suala la kufanya shughuli
zao kwa kuzingatia mifumo ya kileo ya ufanyaji biashara ambayo inauwezo wa
kuongeza thamani biadhaa mbali mbali za matunda na mboga mboga pamoja na kuwepo
mbinu za kileo za uhifadhi bidhaa hizo.
Kwa upande wao wafanyabiashara hao wameomba serikali kuweka mfumo bora wa
utoaji wa elimu kwa wajasiri amali mbali mbali waliopo masokoni ikiwa ni pamoja
na kuwezeshwa kuzisindika na kuzihifadhi kwa njia za kisasa bidhaa za matunda
na mboga mbaga ambazo Zanzibar huwepo kwa wingi katika msimu.
Wamesema kutokana na hali hiyo ya
kukosa elimu na uwezo wa kuifadhi baadhi ya matunda na mboga mboga zimekuwa zikiaribika
na kutupwa kwa baadhi ya wakati kwa kutokuwa na soko na kuleta hasara kubwa kwa
wafanyabiasara jambo ambalo linaweza
kuzuilika kwa elimu na uwezo wa kuzisarifu kisasa bidhaa hizo.
Wameyataja mazao hayo ya msimu kuwa
ni pamoja na embe, tungule, machungwa, ndimu, nanasi na mengine mengi ambayo
iwapo ungekuwepo uwezo wa kuyahifadhi yangeweza kuwa na tija zaidi kwa wakulima
na wafanyabaishara kwa jumla.
Aidha wameomba pia kupatiwa elimu ya
masoko pamoja na kuunganishwa katika mifumo ya masoko mbali mbali duniani
katika kuhakikisha kwamba shughuli hizo za kibiashara zinakwenda vyema na kuwa
na tija kwao.
Mwisho
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Kitengo chake cha Habari leo
Jumanne tarehe 12,Novemba 2024.
No comments:
Post a Comment