Serikali itaendelea kuzingatia ushirikishwaji wa masuala ya kijinsia kufikia Mpango wa Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030 katika nyanja ya sera, bajeti, ufuatiliaji na tathmini na kuhakikisha nchi inafikia mustakabali wa kutoa fursa, usawa, na utu kwa Watanzania wote.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 12 Novemba, 2024 Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Sakina Mwinyimkuu kwa niaba ya Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, na Uratibu), Bw. Anderson Mutatembwa wakati akifungua warsha ya siku tatu ya Ujumuishi Masuala ya Usawa wa Kijinsia na Kijamii katika Ripoti za Tathmini ya Kitaifa ya Hiyari za utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (UN – SDGs Voluntary National Reviews).
Mkurugenzi huyo alibainisha kwamba warsha hiyo imewakutanisha wadau muhimu kutoka Serikalini kupitia Wizara za kisekta, Mashirika ya Kimataifa yakiwemo UN Women, UNDP, UNA, UNICEF na Asasi za Kiraia ili kuimarisha mbinu za nchi katika utoaji wa ripoti za maendeleo endelevu jumuishi hatua inayoonyesha utayari wa Tanzania wa kuongeza juhudi na ushirikiano katika kushughulikia masuala hayo muhimu ya maendeleo.
“Mkutano huu unaonyesha dhamira yetu ya pamoja katika kusimamia ipasavyo Agenda ya Maendele Endelevu ya mwaka 2030 ambayo imejitanabaisha kutokuacha mtu yeyote katika safari ya kufikia maendeleo endelevu hasa wakati huu ambapo nchi ipo katika mchakato wa kuandaa Dira ya Pili ya Maendeleo ya Taifa 2050,” Alisema Bi. Sakina.
Pia alieleza kwamba kufanyika kwa warsha hiyo itakayoendelea hadi Novemba 14, inatoa jukwaa la kipekee kwa wadau kushirikishana uzoefu na mbinu bora katika utoaji wa ripoti za maendeleo jumuishi pamoja na kufanyika kwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalam ili kuimarisha ujuzi wa namna ya kuandaa mipango na bajeti yenye kuzingatia usawa wa kijinsia.
Aidha aliishukuru Tume ya Mipango nchini kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu kufanikisha warsha hiyo pamoja na Taasisi ya Ford Foundation ya nchini Marekani kwa kufadhili mafunzo hayo akisema ni hatua kubwa katika kujitolea kwa Tanzania kwa maendeleo jumuishi na mifumo ya uwazi ya utoaji ripoti.
*MWISHO*
No comments:
Post a Comment