Habari za Punde

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Philip Mpango Atembelea Banda la Tanzania COP29

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akitembelea Banda la Maonesho la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa 29 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) unaofanyika katika Mji wa Baku nchini Azerbaijan. Tarehe 12 Novemba 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewasihi viongozi na washiriki wote wa COP29 kutoka nchini Tanzania kutumia vema fursa waliyopata kwa kuhakikisha Tanzania inanufaika na mkutano huo.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati alipotembelea Banda la Maonesho la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa 29 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) unaofanyika katika Mji wa Baku nchini Azerbaijan.

Amewahimiza kushiriki kikamilifu na kuongeza maarifa ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Amesema ni muhimu pia kuipa kipaumbele ajenda ya nishati safi ya kupikia ambayo Tanzania na Afrika kwa ujumla imedhamiria kutekeleza ajenda hiyo.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewasihi washiriki hao kutoka Tanzania kuwa mahiri katika majadiliano watakayoshiriki katika changamoto za kimazingira zinazoikabili Tanzania na dunia kwa ujumla na suluhu zinazohitajika.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa International Energy Agency (IEA) Dr. Fatih Birol, mazungumzo yaliyolenga kuimarisha ushirikiano katika kutekeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia.

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais. 12 Novemba 2024 Azerbaijan.







No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.