Innalilahiwainnailayhiraajiuun. Mohammed Salum aliyewahi kuwa kocha na captain wa timu ya Shangani ametangulia mbele Allah ampe qauli thabit na amsameh makosa yake na awape subira wana familia yake.
Na.Ally Saleh Alberto.
Naweza kusema Muhammed Salum alikuwa ni mmoja ya wachezaji waanzilishi wa Shangani.
Kwa vile Shangani ilikuwa ni muunganiko ulioletwa pamoja ili kupata timu moja yenye nguvu yeye alitokea Annur. Timu nyengine zilikuwa Spurs na New Star.
Muhammed, au Kocha Muhammed lilokuwa jina la kudumu, yaani marehemu, alifanya uthubutu kwa vile najua ni katika wachezaji wachache kutoka Annur waliokubali kuhamia Shangani hapo 1977.
Ikatokea kwa sababu hio Shangani na Annur kuwa ni mahasimu wakubwa sana kuwahi kutokea katika rekodi ya soka ya Zanzibar na DERBY yao haikuwa ya mchezo.
Muhammed Salum akicheza muda wote nafasi ya beki wa kushoto. Na katika uchezaji wake alishiriki kupata ubingwa kama wa Kombe la FRELIMO na kombe maarufu la Orbit ambapo Shangani iliifunga Black Fighters hapo Amaan Stadium
Katika umri wake akiwa msaidizi kocha alipata raha ya ubingwa wa Zanzibar uliochukuliwa na Shangani FC msimu wa 1993/94...jasho na damu yake ilikuwemo.
Shangani kwa ubingwa huo ilishiriki ubingwa wa Afrika mashariki huko Sudan na kumaliza nafasi ya 3...yeye hata hivyo hakusafiri na timu
Kama kuna ndoa ya mke mmoja ya kudumu maisha yote basi ilikuwa ya marehemu Muhammed Salum na Shangani yake, ambaye mara alikuwa kocha mkuu wa muda lakini mara nyingi akafanywa kocha msaidizi na bila nongwa akatumika.
Amekuwa kocha msaidizi Shangani chini ya Said Humoud, Muhammed Khamis Dingo, Hafidh Badru, Sunday Manara, Madadi, Abdulghani Msoma na wengine...muda wote yupo....na hakika akitoa chake cha mfukoni kwa ajili ya timu.
Marehemu anatoka familia ta michezo....mdogo wake Hafidh amekuwa na historia kubwa pia kwenye ukocha na kufundisha timu pamoja na Pamba ya Mwanza na za ligi Unguja na Pemba.
Mdogo wake Feisal wa guu la kushoto amecheza timu kubwa za Zanzibar na pia kutinga Zanzibar Heroes na Taifa Stars
Akiitwa Feisal Salum...kumbe alikuwepo nyota wa jina hilo kabla Fei Toto
Ameuguwa muda mrefu mpaka Mola alipomhitaji na tumuombee makazi mema myumbani kwake kwa kudumu.
Ally Saleh Alberto
No comments:
Post a Comment