Habari za Punde

Waziri Mkuu Mhe.Majaliwa Akagua Ukarabati na Ujenzi wa Viwanja vya Amani,Maisara na Mao Zedong Zanzibar.Michuano ya AFCON na CHAN Itaendeleza Michezo na Utalii Nchini

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka  kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Tabia Maulid Mwita alipokagua   ujenzi na ukarabati wa viwanja vya Amani, Maisara na Mao Zedong Zanzibar, Aprili 7, 2025. 
Muonekano wa Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Mao Zedong ambao Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikagua ukarabati wake, Aprili 7, 2025
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza  na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Tabia Maulid Mwita    alipokagua  ujenzi na ukarabati wa viwanja vya Amani, Maisara na Mao Zedong Zanzibar, Aprili 7, 2025.
Waziri Mkuu, Kasssim Majaliwa akikagua sakafu ya uwanja wa Ndani wa Amani wakati alipokagua ujenzi na ukarabati wa viwanja vya Amani, Maisara na Mao Zedong Zanzibar, Aprili 7, 2025. 
Muonekano wa Uwanja wa Mpira wa Miguu Amani Zanzibar ambao Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikagua ukarabati wake, Aprili 7, 2025.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukagua ujenzi na ukarabati wa viwanja vya Amani, Maisara na Mao Zedong Zanzibar, Aprili 7, 2025.
 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Mhe. Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi wa kuridhia Mashindano ya AFCON na CHAN kufanyika nchini utasaidia kwa kiasi kikubwa kuendeleza na kukuza sekta ya michezo na utalii nchini. 


Akizungumza baada kukagua ukarabati na ujenzi wa Viwanja vya Amani, Maisara na Mao Zedong Zanzibar leo Aprili 7, 2025, Mheshimiwa Majaliwa amesema Watanzania watapata fursa ya kuendeleza michezo na kuhamasisha wachezaji kufanya mazoezi zaidi ili wapate sifa za kucheza michuano hiyo.


“ujio wa wageni wakati wa michuano utahitaji malazi, chakula na usafiri  hivyo waliowekeza kwenye hoteli na vyombo vya usafiri watapata faida kubwa na kujiingizia kipato, hii ni fursa nzuri ambayo Marais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi wametuletea kwa sababu timu zinakuja na watu wengi.”


Aidha Mheshimiwa Majaliwa amesema ameridhishwa na kasi na bora wa ukarabati wa viwanja hivyo unaofanywa na kampuni za REFORM na ORKUN “Kampuni hizi zimetujengea viwanja vilivyo na ubora  unaokubalika”.


Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa jukumu lililopo kwa sasa  ni kuilinda miundombinu hiyo  ili ubora uliofikiwa  baada ya ukarabati uendelee kuwepo hadi michuano hiyo itakapofanyika “Watanzania wanatamani kuvitumia  viwanja hivi lakini wanatakiwa wajue kwamba viwanja hivyo kwa sasa viko kwenye ukaguzi maalum  unaofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika hivyo ni muhimu  kuweka utarabu ambao hautaathiri ubora ulipo”.


Pia amesema kuwa pale inapobidi  serikali hawatazuia viwanja hivyo kutumika katika michezo mikubwa ila kinachotakiwa ni kufanyika kwa ukarabati wa mara kwa mara baada ya matumizi ili kulinda ubora wake utakaoiwezesha nchi kukidhi vigezo vya kuendesha mashindano hayo .


Pia, Waziri Mkuu amesema mashindano hayo yataleta manufaa makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya utalii na biashara. "Hii ni fursa nzuri ambayo Marais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi wametuletea kwa sababu timu zinakuja na watu wengi.”


Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Tabia Maulid Mwita na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni , Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa ni miongoni mwa viongozi waliombatana na Waziri Mkuu katika ukaguzi wa viwanja hivyo.


Mwisho

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAPILI, APRILI 7, 2025



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.