Habari za Punde

MASHEHA NI MUHIMU KATIKA KUDUMISHA UTAWALA BORA

Na Halima Abdalla

NENO Sheha si msamiati mgeni katika mazingira ya Zanzibar kwani inasadikika kwamba neno hili lilikuwepo miaka mingi iliyopita na lilikuwa linatumika kwa maana sawa au inayokaribiana na maana iliyopo sasa.

Katika kipindi cha hivi karibuni neno Sheha au Shehia limepata umaarufu mkubwa kutokana na kupewa nguvu ya kisheria na kuainisha majukumu ya mtu anaepata dhamana kuwa Sheha wa Shehia fulani.

Hali hii imesaidia sana kupanua wigo wa neno Sheha kiais kwamba kwa sasa katika mazingira ya Zanzibar ni wachache sana ambao hawajapambana aidha moja kwa moja na Sheha mwenyewe au wajumbe wa kamati ya Sheha wanapokuwa wakitimiza majukumu yao ya kikazi.

Ili kuwepo mfumo mzuri wa utendaji kazi wa Masheha ,Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mnamo mwaka 1998 ilipitisha sheria Namba 1 ya mwaka 1998 kwa lengo la kuongoza na kusimamia utawala wa Serikali kuu katika ngazi ya Shehia na kuweka madaraka karibu zaidi na wananchi.

Aidha sheria hii pamoja na mambo mengine imekuja kutandika mfumo mzuri zaidi wa kusimamia uendeshaji wa shughuli za Serikali kuu katika Mikoa, Wilaya na Shehia.

Lengo kuu la mfumo huu ni kuweka huduma za jamii karibu na wananchi na kupanua wigo wa ushirikishwaji kwa mujibu wa sheria hii NO.1 ya mwaka 1998, kifungu cha pili cha sheria hii, kinatoa tafsiri ya maneno na miongoni mwa maneno yaliyotafsiriwa chini ya kifungu hichi ni pamoja na neno Sheha ambapo kifungu kinatafsiri neno Sheha kama ni Afisa aliyechaguliwa chini ya kifungu cha 15 cha sheria hii.

Kamishna wa Wizara ya Kazi Uwezeshaji wananchi kiuchumi Kubingwa.M.Simba alisema kila shehia inaongozwa na Sheha ambaye anachaguliwa na Mkuu wa Mkoa kwa kushauriana na Mkuu wa Wilaya .

Alisema sheria ikienda mbali zaidi katika kifungu cha 16 kwa kuweka bayana sifa za Sheha kwa kusema hakuna mtu atakae chaguliwa kuwa Sheha mpaka awe kwanza Mzanzibari, Mtu anayeheshimika katika jamii, mwenye tabia nzuri, mwenye umri usiopungua miaka 40 na ambae anaelimu ya msingi na anajua kusoma na kuandika.

Alisema Sheha katika Shehia anakazi ya kusimamia sheria zote, maagizo ya Serikali, sera na maelekezo mengine kwa ajili ya utekelezaji wa sheria.

Alifahamisha kazi nyengine za Sheha ni kusuluhisha migogoro ya kijamii na kifamilia katika shehia yake kwa mujibu wa utamaduni na mila za eneo husika.

Kutunza kumbukumbu zote zinazohusiana na usajili wa ndoa, talaka, kizazi na vifo, ruhusa ya ngoma, kusafirisha mazao, mifugo, makaa kama itakavyoelekezwa na mamlaka husika.

Alieleza kazi nyengine ya Sheha ni kudhibiti uhamiaji katika eneo lake na kuweka kumbukumbu pamoja na kupokea taarifa za mikutano ya hadhara katika shehia yake na kufanya shughuli nyengine yoyote halali kama atakavyotakiwa na Mkuu wa Wilaya.

Sheria pia inasisitiza kwamba kila Sheha atawajibika kwa Mkuu wa Wilaya ambae Shehia yake ipo.

Aidha sheria hii inawataka watu wowote ambao wanadhamiria kuhamia katika Shehia kama wakaazi wapya basi watoe taarifa kwa Sheha husika.

Katika kutekeleza lengo hilo, Sheria inatoa adhabu kwa mtu yeyote atakaekiuka masharti ya kifungu hiki cha sheria atakuwa amefanya kosa na iwapo atatiwa hatiani atapata adhabu ya kulipa faini isiyopungua shilingi 30,000/= au kifungo cha siku thalathini au adhabu zote kwa pamoja.

Kwa mantiki hii tunaweza kubaini kwamba Sheha ni kiongozi wa Serikali katika Shehia ambaye anatambuliwa kisheria na amepewa mamlaka ya kisheria kusimamia uendeshaji wa shughuli za Serikali katika eneo lake la kazi .

Mbali na hayo, Sheria hii imekwenda mbali zaidi kwa kutoa adhabu pia kwa wale wote watakao kwenda kinyume na baadhi ya vifungu vya sheria hii.

Dhana ya Utawala Bora ni dhana pana ambayo ni vigumu kupata tafsiri yake ya moja kwa moja. Kutokana na hali hiyo, wanaharakati wengi wa Utawala bora wamekuwa wakitoa tafsiri mbalimbali juu ya dhana hii.

Wapo wanaoamini utawala Bora ni utawala wa Sheria kuzingatia haki za binadamu,kupiga vita rushwa,Demokrasia na ushirikishwaji wa jamii katika kuleta maendeleo,kuzingatia misingi ya uwazi,uwajibikaji,haki na kuheshimu maamuzi ya wengine pamoja na mgawanyo sawa wa rasilimali za nchi baina ya watu wake.

Kwa Upande wake Kamishna Simba alisema kwa ujumla Utawala bora unatazamwa kama mfumo mzima wa Uongozi ,kitaasisi, kimuundo, kimchakato, kitaratibu , kimahusiano na kitabia ambao unawapa uwezo watawaliwa kuamua nani awatawale na namna ambayo wanataka vyombo vya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutawala visimamie masuala ya umma.

Alisema pamoja na kutokuwepo tafsiri ya moja kwa moja ya Utawala Bora kama nyumba inamisingi ambayo kukamilika kwake kwa ujumla ndio kunajenga huo utawala bora.

Alifahamisha kuwa katika msingi huu wa Utawala bora inatarajiwa kwamba kila mtu popote alipo, kikundi cha watu,taasisi zisizokuwa za Kiserikali zitimize wajibu wake.

Alisema hivyo basi katika Utawala bora watumishi wa umma pia wanatakiwa wawepo katika nafasi zao za kazi kwa wakati na kuwajibika katika kiwango cha juu ili jamii ipate huduma kwa wakati na kwa kiwango kinachotarajiwa.

Umuhimu wa Utawala bora katika jamii unapoimarika katika jamii,kunapelekea kuwepo kwa amani na utulivu,umoja wa kitaifa, usalama wa wananchi na mali zao.

Suala la Utawala bora si la Serikali peke yake kama wengi wanavyodhani serikali siku zote ni muhimu kwa kuweko kwa kuweka mazingira mazuri ya Utawala bora kisheria, kisera na kuhudumia jamii katika masuala ambayo haiwezi kuyaacha kwa sekta binafsi.

Katika kuhakikisha kuwa Utawala Bora unajengwa kwa kudumishwa kuanzia ngazi ya familia hadi taifa kuna taasisi zenye mchango mkubwa katika kuimarisha utawala bora nchini .

Wizara ya Nchi Afisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala bora ,Wizara ya Nchi Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Vyombo vya sheria kama vile Mahkama, Afisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Afisi ya mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, vyombo vya kidini, Baraza la Wawakilishi na Tume ya Uchaguzi, jumuia na Mashirika yasio yaki Serikali ya Kitaifa na Kimataifa pamoja na Sekta binafsi na vyombo vya habari.

Kamishna wa Kazi Kubingwa alisema pamoja na kwamba kila mtu anajukumu kubwa katika kudumisha Utawala bora hapa Zanzibar, lakini Masheha wanajukumu mahsusi katika kufanikisha Utawala bora.

Alisema masheha wananafasi kubwa kwa sababu kwa lugha nyepesi wao ndio wanao simamia watu katika maeneo yao na hivyo mabadiliko yeyote katika jamii yanatakiwa yaanzie kwao.

Katika kufanikisha Utawala bora Masheha wanatakiwa kufanya kazi kwa uwazi,kuwashirikisha wanashehia,kufuata sheria,kuepuka rushwa na kufanya kazi kwa usawa kwa wote.

Pamoja na hatua hizi zinazopendekezwa katika kuimarisha ufanyaji kazi wa masheha ili kuimarisha Utawala bora hapa Zanzibar kwa ujumla, Masheha wanatakiwa pamoja na mambo mengine kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya Utawala bora.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.