Habari za Punde

JAMP YAHAMASISHA UHIFADHI MAZINGIRA

Na Zuwena Shaaban, Pemba

JAMII imeshauriwa kutilia maanani suala zima la uhifadhi mazingira ili waweze muepukana na maradhi mbali mbali yanayoweza kutokana na uharibifu huo.

Kaimu Katibu wa Jumuia ya kuhifadhi mazingira na upandaji wa miti (JAMP), Salum Said Ali, iliyoko Pondeani Shehia ya Kibirizi katika Wilaya ya Chake Chake wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hii.

Alisema suala la uhifadhi wa mazingira linakabiliwa na changamoto nyingi hasa katika kipindi hichi cha mvua ikiwemo kujiepusha na maradhi ya kuambukiza ambayo hutokana na kuchafua kwa mazingira.

Katibu huyo alisema lengo la Jumuia hiyo ni kuhakikisha inahamasisha jamii juu ya suala zima la uhifadhi mazingira na kuondosha maambukizi ya kipindupindu, kichocho na homa za matumbo.

Alisema watoto wao wako hatarini kutokana na maji hayo kuchotwa na kuwekwa majumbani kwa ajili ya baadhi ya shughulu lakini watoto hao baadhi ya wakati hufika kunywa maji hayo kutokana na uelewa wao mdogo.

Alieleza licha ya kujipanga kuweka mazingira safi lakini kuna baadhi ya watu wanakaidi na suala la usafishaji wa mazingira na kupelekea kuzagaa kwa uchafu na huku ikawa sambamba na ukataji wa miti.

“Tunapanda miti lakini mtu anathubutu kukuambia hapo usiupande ukiupanda basi nitaukoa na anaukoa kweli kutokana na akili finyu aliyonayo kwani sisi tunapanda kwa ajili ya kuweka mazingira safi na wala sikwajambo jengine lolote lile lakini mtu huyo anathubutu kuung’oa ,kwa kweli suala hili ni tatizo sana kwetu na inatuwia vigumu kusonga mbele”,alileza Kaimu Katibu.

Naye Mjumbe wa kikundi hicho Raya Said Seif alisema kama wao wanawake wanakabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo ukosaji wa vifaa vya kusafishia na kudharauliwa na baadhi ya wanajamii hao kutokana na kushiriki katika kuhifadhi mazingira yaliyowazunguka.

Pia wanaziomba taasisi zinazohusika na uhifadhi mazingira kuweza kuwatembelea na kuwa pamoja katika kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na kuweza kupiga vita maradhi ya miripuko kwani kijiji hicho kiko hatarini na maradhi hayo kutokana na uchafuzi wa mazingira.

Jumuia ya JAMP iliazishwa mwaka 2007 na kupata usajili rasmi mwaka 2008 na kuweza kuanza na wanachama saba ambapo kwa wakati huo walikuwa wote ni wanaume lakini kwa sasa jumuia inawanachama 20 wakiwemo wa kike na wakiume.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.