UTAFITI wa Demografia na Hali ya Afya Tanzania 2010, Zanzibar umegundua uwepo wa mitazamo finyu katika jamii kwa wanandoa hususani akinamama kwamba wana haki ya kupigwa na waume zao pindi wanapowanyima tendo la ndoa au kuunguza chakula.
Akiwasilisha mada ya uwezeshaji wa wanawake, ukatili wa kijinsia na Ukeketaji, Wahida Maabad kutoka Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, amesema matokeo ya utafiti huo nchini yameonesha wanawake waliohojiwa wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 kwamba waume wana haki ya kuwapiga wakiunguza vyakula au kuwanyima tendo la ndoa.
Alieleza takwimu zinaonesha kwamba kwa Tanzania Bara asilimia 18 wamekubali kupigwa wakiunguza chakula wakati Zanzibar kwa asilimia tano.
Aliongeza kusema kwamba, asilimia 30 Tanzania Bara wamethibitisha waume wana haki ya kuwapiga wake zao pindi wakikataa kujamiiana (tendo la ndoa) na mtazamo huo kwa Zanzibar ni asilimia 12 na asipohudumia watoto waliokubali kichapo asilimia 40 Tanzania Bara na Zanzibar asilimia 15.
Aidha alisema wakibishana na waume zao wamekubali kupigwa kwa asilimia 39 kwa Tanzania Bara na Zanzibar asilimia 13 na kosa la kutoka bila ya kumuaga mumewe asilimia 37 Tanzania Bara walikubali na Unguja na Pemba kwa asilimia 19.
Hata hivyo alieleza dhana hiyo kwa waume ipo tofauti na wanawake waliohojiwa katika utafiti huo, ambapo asilimia 14 kwa Tanzania Bara na Zanzibar asilimia tisa ndio waliokubali kwamba wana haki ya kumpiga mke pindi akikataa kujamiiana naye, kiwango ambacho ni kidogo ukilinganisha na walivyokubali wanawake kwa asilimia 30.
Muwezeshaji huyo, alisema kutokana na utafiti huo bado kunahitajika elimu katika jamii ili kuondosha kasoro hizo zisiendelee kuwepo, ambapo alisisitiza asilimia 15 imeonesha kwamba ukeketaji bado upo nchini Tanzania katika mikoa ya Manyara, Arusha, Singida na Dodoma ambayo ipo juu katika masuala hayo.
Nae Dk. Aza alitoa mada ya uzazi wa Mpango alisema wanawake wasioolewa wanajihusisha na tendo la ndoa wanaotumia zaidi njia za uzazi wa mpango kwa takribani ya asilimia 45, ambapo asilimia 16 wanatumia mipira ya kiume na asilimia 15 wanatumia sindano nchini ukilinganisha na walioolewa wanatumia kwa asilimia 27 kwa Tanzania na asilimia 12 kwa Zanzibar. Alisema njia za uzazi mpango unamuwezesha jinsi ya upangaji wa watoto na kuweza kuwalea vizuri pamoja na mama kuwa na afya njema.
No comments:
Post a Comment