Na Mwandishi Wetu
VYOMBO vya habari vina wajibu wa kuwaunganisha wananchi Zanzibar, umuhimu wa kuwa na serikali ya Umoja wa Kitaifa, hasa baada ya wananchi hao kupita katika kipindi kigumu na cha muda mrefu cha hitilafu za maelewano zilizotokana na hali ya siasa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alieleza hayo jana alipokuwa akitoa mada kwenye warsha ya siku mbili inayoelezea nafasi ya vyombo vya habari katika kuimarisha serikali ya Umoja wa kitaifa.
Mhadhiri huyo alisema kihistoria Zanzibar imepitia katika mkondo mrefu wa wa kuhitilafiana kisiasa, hali ambayo imezikwa na maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa baina ya vyama vya CUF na CCM.
Alifahamisha kuwa baada ya kupatikana kwa serikali ya Mapindui ya Zanzibar iliyo katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa, ambayo imekuwa msingi imara wa utengamano baina ya Wazanzibari hivi sasa umefika wakati wa kuzienzi na kuzitunza tunu za taifa.
Alizitaja tunu hizo ambazo hazijawekwa katika utaratibu mzuri na baadhi yao zinahitaji kufanyiwa mapitio ni pamoja na amani, umoja,, uzalendo, mshikamano, usawa, haki, muungano, uvumilivu katika dini, rangi na siasa.
Muwezeshaji huyo alisema jamii ipaswa kuelimishwa kwa undani umuhimu wa tunu hizo ambazo zina umuhimu mkubwa katika kujiletea maendeleo, na kueleza kuwa kazi hiyo inaweza kufanywa kwa usahihi na vyombo vya habari.
Kwa upande wake Rashid Omar Kombo ambaye ni Mhadhiri wa Chuo cha Habari Zanzibar, akiwasilisha mada katika warsha hiyo alisema vyombo vya habari vinawajibu wa kuitathmini hali ya utawala bora kwa kutumia viashiria vilivyopo hasa wakati huu ambapo Zanzibar ina serikali ya umoja wa Kitaifa.
Alisema utawala bora una mchango mkubwa katika kukuza maendeleo ya nchi yoyote sambamba na upatikanaji wa haki za msingi ambazo kila mwanadamu anatarajiwa kuzipata bila ya kuwepo mizengwe yeyote.
Wakichangia washiriki wa warsha hiyo walipendekeza uwepo uwajibikaji wa vyombo vya habari katika kutoa taarifa sahihi kwa wasikilizaji, wasomaji na watazamaji wa vyombo vyao na kutaka uweledi utumike ili kuepusha kuandika habari zinazoweza kusababisha mifarakano katika jamii.
Awali akifungua warsha hiyo waziri wa Biashara na Viwanda, Nassor Ahmed Mazrui, kwa niaba ya waziri wa Habari, Utamaduni Utalii na Michezo, Abdilahi Jihad Hassan, alivitaka vyombo vya habari viandike habari zao kwa misingi ya uweledi ili kuepuka kuwa msingi wa mitafaruku katika jamii.
Waziri huyo alisema umefika wakati wananchi kuelimishwa na kuzielewa tunu za taifa ikiwemo Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964, ambayo ndiyo yaliyomkomboa kila Mzanzibari.
Waziri Jihad Hassan alivitaka vyombo hivyo viandike habari zao kwa misingi ya uweledi ili kuepuka kuwa msingi wa mitafaruku katika jamii na kueleza kuwa Zanzibar tuitakayo inaweza kujengwa na wazanzibari wenyewe.
Warsha hiyo ya siku mbili inawashirikisha waandishi wa habari, watendaji wa vyama vya siasa pamoja na taasisi za kiraia, na imeandaliwa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET).
No comments:
Post a Comment