Habari za Punde

MSAKO MADAKTARI WALIOAJIRIWA KINYEMELA WAANDALIWA

Na Fatma Kassim, Maelezo

BODI ya ushauri ya hospitali binafsi imegundua kuwepo kwa madaktari na wauguzi wanaotoka Tanzania Bara ambao wanafanya kazi katika mahoteli ya kitaalii ambao hawajajisajili katika bodi hiyo kwa ajili ya kufanya kazi zao za kidaktari.

Madaktari hao wamebainika kufanya kazi hizo katika mahoteli makubwa yaliopo katika sehemu za shamba na mijini Zanzibar ambayo hufika watalii kwa ajili ya kupumzika na kufanya shughuli zao za kitalii.

Msaidizi Mrajis wa Bodi ya ushauri ya Hospitali Binafsi, Dk. Shaaban Seif Mohammed, alisema kutokana na kuwepo kwa hali hiyo bodi yake inaratajia  kufanya msako kupita kila hoteli na wakiwabaini madaktari wa aina hiyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa zidi yao.

Alisema mbali ya kuwepo kwa madaktari hao pia wamegundua kuwepo kwa wauguzi ambao wanafanya kazi za kidaktari katika mahoteli hayo jambo ambalo si sahihi kwa maaduli ya kazi za kiafya pamoja na kuwa wauguzi pamoja na madaktari kuwa hawana sifa za kifanya kazi hizo.

Aliwataka madaktari hao kufika katika bodi yao kufanya usajili na kuendelea na kufanya kazi zao za kidaktari  na wauguzi kufika katika baraza la wauguzi kujisajili ili waweze kutambulika kisheria kulingana na taaluma zao na Bodi hiyo haubagui wafanyakazi wanaotoka Tanzania Bara na badala yake inataka watanzania wote wafuate sheria za nchi zinavyoelekeza.

Dk. Shaaban alifahamisha kuwa kutokana na wamiliki wa mahoteli wanatambua kuwepo kwa hali hiyo Bodi yake imetoa tahadhari kwa wamiliki kuacha kabisa vitendo hivyo na kufuata taratibu za Bodi ili lengo lifikiwe la kutoa huduma bora za afya.

Katika hatua nyengine Bodi yake imewataka wamiliki wa hospitali binafsi kufuata taratibu zilizowekwa na bodi hiyo ikiwemo ya kuweka usafi hospititali zao, kuwa na madaktari wenye sifa pamoja na kuhifadhi vizuri dawa zao pamoja na kuwa na vifaa vya kuchunguzua vyenye uhakika na vyenye ubora wa hali ya juu.

Alisema kufanya hivyo kutaweza kufanikisha utendaji wa mzuri wa afya za wananchi kwani hospitali binafsi zinasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano katika hospitali mbali mbali za Serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.