Habari za Punde

WANAWAKE HATARINI KUBABUKA NYUSO

Na Mwantanga Ame

BAADHI ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamedai wanawake wengi wako hatarini kubabuka nyuso zao kutokana na kutumia vipodozi ambavyo hawafahamu maelezo ya lugha iliyotumika kuelezea matumizi yake.


Mwakilishi wa Wanawake Mwanajuma Faki Mdachi, aliyasema hayo akichangia bajeti ya Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, iliyowasilishwa na Waziri Nassor Ahmed Mazrui, katika ukumbi wa Baraza hilo Visiwani Zanzibar.

Mwakilishi huyo alisema hivi sasa wanawake wengi wa Zanzibar wamekuwa wanajichubua ngozi zao na wapo hatarini kufanya mabaka ya usoni kutokana na baadhi yao hupaka vipodozi hivyo bila ya kujua matumizi halisi yaliyokusudiwa.

Alisema tatizo hilo limekuwa likichangiwa na lugha inayotumika kuwa ni ya kiingereza huku baadhi yao kutoifahamu jambo ambalo husababisha kutoyaelewa vyema matumizi halisi ya vipodozi hivyo.

“Wazanzibari wanajichubua hali zao zimebadilika nyusoni vipodozi vinaandikwa kiingereza hawavijui wanatumia matokeo yake wanaungua nyuso sasa hivi wamejaa mabaka” alisema Mwakilishi huyo.

Alisema ili kukabiliana na tatizo hilo ni vyema serikali ikaweka utaratibu kwa wafanyabishara wanaoingiza vipodozi hapa nchini kuwawekea utaratibu utaokuwa unawataka waingize vile ambavyo vitakuwa na lugha inayofahamika hasa ya Kiswahili.

Hatua hiyo, alisema itasaidia kuwawezesha watumiaji hao wa vipodozi kuyafahamu matumizi halisi wanayotakiwa kuyafanya kwa vipodozi hivyo

Wakati huo huo, Mwakilishi wa Matemwe, Abdi Mosi aliiomba Wizara hiyo ya biashara kufikiria kuanzisha viwanda katika maeneo ya vijijini ambavyo vitakuwa vinazalisha maji, samaki, kukausha madagaa.

Aidha Mwakilishi huyo aliiomba Wizara hiyo kufikiria kuwapatia mikopo wafanyabiashara wa dogo wadogo kutokana na hivi sasa kuonekana eneo hilo linakosa msukumo maalumu.

Nae Mwakilishi wa Konde, Suleiman Hemed akitoa maoni yake alisema ipo haja kurejeshwa kwa maonyesho ya biashara pamoja na soko la Jumapili ikiwa ni sehemu ambayo itayoweza kukuza masoko kwa wafanyabiashara za Zanzibar.

Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, alisema Wizara itapaswa kuliangalia suala la uwepo wa utitiri wa leseni wanazokatishwa wafanyabiashara kutokana na hivi sasa kumsababishia mzigo mkubwa.

Mbarouk Wadi Mtando (Mkwajuni),  aliiomba Wizara hiyo kumpatia maelezo juu ya muwekezaji aliyeachwa kuuziwa karafuu tani 10,000 alietaka kulipia dola za kimarekani 12,000 na badala yake Shirika la ZSTC, ilimuuzia mfanyabiashara mwengine kwa dola za kimarekani 8,000 kwa tani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.