Yaliyoshindwa kujibiwa kuundiwa tume
Waziri kuwanyoosha wavujisha mapato
Na Mwanajuma Abdi
PAMOJA na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuibana bajeti ya Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, hatimaye wajumbe wa Baraza hilo jana waliyapitisha makadirio ya bajeti hiyo kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, alijitahidi kutoa ufafanuzi wa kina na kupongezwa na wajumbe wengi, lakini alikumbana na vigingi vya wawakilishi wakati wa kupitishwa mafungu ya matumizi.
Wakichangia bajeti hiyo, baadhi ya wajumbe wa Baraza hilo walidhamiria kutoiunga mkono bajeti hiyo hadi hapo watakapopatiwa ufafanuzi wa kina kwenye masuala yao ambayo walisema yalionesha utata.
Wakati wa kupitishwa mafungu hayo, Mwakilishi wa Kwamtipura, Hamza Hassan Juma, alisimama na kueleza kuwa bajeti hiyo itapita hasa kwa heshima ya Balozi (Makamu wa Pili wa Rais) na Spika wa Baraza hilo Pandu Ameir Kificho.
“Hakuna wasiwasi bajeti hii itapita kwa heshima Balozi na kwa heshima yako wewe Mheshimiwa Spika”, alisema Hamza.
Baada ya kutoa kauli hiyo aliweka pingamizi na kusema mali za serikali zimekuwa zikiyoyoma na maeneo mengi yanatoweka kiholela na mengine yanachukuliwa kwa nguvu bila ya kufuatwa kwa utaratibu akitoa mfano kiwanja cha Living Stone House kupewa mtu binafsi baada ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kukataa kujenga Ofisi.
Ufafanuzi, Waziri Omar alisema suala hilo hauhusiki na madai hayo kwa vile eneo hilo linamilikiwa na wizara ya Kilimo na waliwasiliana na wizara hiyo pamoja na Idara ya Ardhi, kwa ajili ya kulirejesha eneo hilo.
Alisema kama kapewa mtu binafsi wizara yake haijui, wahusika ni wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati ndio wenye uwezo wa kutoa ardhi kisheria.
Hamza aliendelea na msimamo wake wa kutokubaliana na majibu hayo huku akilalamika tatizo la mawaziri kujichanganya katika utoaji wa majibu na hivyo, kumshauri Spika Kificho Baraza lirejee kwa kutumia kanuni ya kifungu cha BLW cha 117 ili kuweza kuundwa kwa kamati teule ya kuchunguza.
Kwa upande wake waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame alimtaka Mwakilishi huyo akubaliane na hoja kwamba kamati ya Baraza ya Ujenzi na Mawasiliano ipewe kazi hiyo, huku akisema Hamza atashirikishwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, aliridhia suala hilo liingizwe katika kamati teule itayochunguza masuala mbali mbali ya serikali itayoundwa kwa kuwashirikisha wajumbe wa Baraza hilo.
Spika Pandu Ameir Kificho, alisema ni vyema suala hilo likaingizwa katika uchunguzi wa kamati moja ili kupunguza mlolongo wa kamati kwa ajili ya kuepusha matumizi makubwa ya fedha.
Awali katika ufafanuzi wake waziri Omar Yussuf Mzee alisema serikali imetangaza vita kwa watumishi wataojihusisha na uvujishaji wa mapato na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao pindi ikithibitisha ili kufikia malengo ya kuziba mianya hiyo nchini kwa maslahi ya Taifa.
Alisema watumishi watakaojihusisha na kadhia hiyo hatowavumilia, ambapo ikithibitika hatua za kisheria zitachukuliwa kwa mtu yeyote yule atayejiingiza huko.
Alieleza mikakati kabambwe imeandaliwa na serikali ya kuziba mianya ya uvujaji wa mapato katika vyanzo vyake mbali mbali ikiwemo Uwanja wa Ndege na Bandarini, ambapo sio vizuri kuitaja kwa vile wajanja watatumia mbinu nyengine kukabiliana na mikakati hiyo.
Akifafanua kuwa, jengo la Mambo Msiige lililozua mjadala wakati wa upitishaji wa vifungu wa bajeti hiyo, ambapo Mwakilishi wa Mkwajuni, Mbarouk Wadi Mussa (Mtando), aliyetaka ufafanuzi jengo hilo limeuzwa au linamilikiwa na Serikali.
Waziri Omar alieleza kwamba jengo hilo halijauzwa na linamilikiwa na Serikali na linakusudiwa kukodishwa ambapo hadi sasa mikataba bado hawajaingia na huyo atayekodishwa na kilichofanyika kwa sasa ni kukodishwa eneo la ardhi kwa hekta 0.42 kwa Dola za Marekani 10, 000 kwa mwaka na sio jengo hadi alifanyie matengenezo ndio watakubaliana kima cha kukodishwa.
Aidha Mtando alihoji kwa nini wafanyakazi walihamishwa kwa haraka, ambapo hata mikataba ya ukodishwaji wa jengo hilo bado haijafanyika, sambamba na kutaka gharama zilizotumika kuwahamisha wafanyakazi wa hapo na kuwapelekea jengo la zamani la Benki ya Watu wa Zanzibar Ltd. (PBZ).
Waziri Omar alisema kuhamishwa kwa wafanyakazi waliokuwa wakitumia jengo hilo ni kutokana na ubovu wake, jambo ambalo lilikuwa linahatarisha maisha yao na hata Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi alikwenda kulikagua na kuiona hali ya jengo hilo.
Alisema gharama zilizotumika katika kuwahamishia wafanyakazi katika jengo la zamani la PBZ limetumia shilingi milioni nane na limefanyiwa matengenezo kwa shilingi milioni 170.
Hata hivyo, suala hilo lilizua mjadala, hali iliyomfanya Spika wa Baraza hilo, Pandu Ameir Kificho kuingilia kati suala hilo na kuliingiza katika kamati teule itayoundwa katika Baraza la Wawakilishi kuchunguza masuala mbali mbali ya serikali ikiwemo mikataba ambayo imewaonesha utata kwa wajumbe hao
No comments:
Post a Comment