Habari za Punde

TAMKO LA MUWAZA JUU YA KIAPO CHA RAIS WA ZANZIBAR

KATIKA BARAZA LA MAWAZIRI LA MUUNGANO

MUWAZA imepata mshangao na kusikitishwa na hatua ya rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein kuamua kula kiapo kwa minajili ya kuingia katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Tunakiona kitendo hiki kama ni muendelezo wa udhalilishaji kwa Serikali ya Zanzibar pamoja na wananchi wake. Pamoja na kuwa suala hili limetajwa katika katiba ya Muungano, lakini haikuwa ni mazoea kwa ma Rais waliopita kuhudhuria kiapo hiki. 


Kwa mnasaba huo, tunapata masuala mengi kuliko majibu. Ni kwa nini Rais wetu amefanya kitendo hiki wakati huu ambapo utaifa wa Zanzibar unazidi kuchomoza kutokana na muamko, umoja, na nguvu ya Wazanzibari.

MUWAZA inaamini kwamba, masuala yote yanayohusu Zanzibar yatajadiliwa na Wazanzibar wenyewe kupitia Serikali yao na Baraza lao la Wawakilishi. Endapo vyombo hivyo vitashidwa, basi Wazanzibari wenyewe wanayo nguvu yao ya kikatiba kuamua mambo yao kwa kupitia kura ya maoni. Uwezo huo upo na ni hiari ya Wazanzibar kuutekeleza wakati wowote, aidha kwa kutumia katiba iliyopo sasa au ye yote ile ya Muungano itakayokuja. 

Katika hali hiyo, Rais wa Zanzibar anahudhuria katika Baraza la Mawaziri la Muungano kwa
kujadili masuala gani?

MUWAZA inaamini kwamba Rais wa Muungano na Serikali yake ya sasa inayo haki ya kuendesha mambo yote ya Tanganyika na yale yahusuyo Muungano. Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Serikali ya Zanzibar wanayo mamlaka yote ya kushughukilia mambo yahusuyo Zanzibar na pia kazi ya kuhakikisha kuwa
maslahi ya Zanzibar na uhuru wake ndani na nje ya Muungano yanaheshimiwa.

Panapo tokea mvutano, ni wajibu wa Marais wawili kukaa pamoja na kutafuta ufumbuzi kwa kutumia miongozo ya Serikali zao. Kwa vyovyote vile, hakuna  mantiki na si haki kwa Baraza la Mawaziri la Muungano kujadili na kuamua mambo mazito yanayohusisha masuala muhimu ya Zanzibar ati tu kwa sababu
Rais wa Zanzibar amehudhuria au ni mwanachama katika Baraza hilo. Kiini macho hicho hakikubaliki.

MUWAZA inamnasihi Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, Dk. Mohammed Ali Shein, kuchukua hatua za haraka za kuwafahamisha Wazanzibari juu ya uamuzi wake wa kuhudhuria kiapo hiki hasa kwa vile hakuomba ridhaa yao kabla ya kutenda kitendo hicho. 

Aidha, tunamkumbusha juu ya umuhimu na mamlaka aliyonayo akiwa kama Rais wa Nchi kamili inayozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hatuoni sababu ya Rais wetu kuhudhuria katika Baraza la Mawaziri la Muungano akiwa aidha kama waziri au Rais wa Zanzibar. Hatutegemei kumuona anaendelea kuhudhuria vikao hivyo.

Venginevyo, tutakilaani kitendo chake hiki kwa nguvu zote.

Kwa niaba ya MUWAZA
Dr. Yussuf S. Salim
Mwenyekiti
Copenhagen
Denmark
31.10.2011

8 comments:

  1. Kwanza nahisi huyu Dr Yussuf yeye si mzanzibari na wala hakupiga kura kumchagua Dr Shein kwahiyo hakupaswa kujifanya kuwa yeye ni mwakilishi wa wazanzibari na wala hakupaswa kumuelekeza raisi nini cha kufanya. Ilikuwa ni jukuma la wapiga kura kufanya hivi.
    Pili hoja ya kuwa huko nyuma maraisi waliopita hawakuwa wakihudhuria vikao hivi kwahiyo hayakuwa mazoea hii sio hoja yenye nguvu.
    Mwisho Dr Shein hakupaswa kuomba ridhaa ya watu kuhudhuria vikao hivi. Ridhaa alishapewa pale alipopigiwa kura.

    ReplyDelete
  2. Tatu pale marekebisho ya Katiba yalipopitishwa kumfanya Rais wa Zanzibar kuwa Mjumbe katika Baraza la Mawaziri la Muungano ni Wabunge Wetu kutoka Zanzibar waliopitisha Muswada na kuuwafiki.

    Sijui kama Sheria hii ilihitajia kupata Baraka za Baraza la Wawakilishi au vyenginevyo

    ReplyDelete
  3. NAONA KAMA UMEKOSEA KITU MTOA COMMENT AU NAWEZA KUSEMA UMEPITIKIWA ILA NATAKA KUKUMBUSHA TU, KUKAA NJE YA ZANZIBAR AU KUTOPIGA KURA SI KAMA NDIO UZANZIBAR WAKO UNAFUTIKA....NAKUOMBA TU UKIANDIKA KITU ANDIKA KWA POINT HATA MIE NAWEZA KUSEMA KWA MUANDIKO HUU BASI INAONYESHA HUJAPITA SKULI AU HUNA AKILI.

    ReplyDelete
  4. Dr. Yussuf ,

    Nimeipokea risala ya Tamko la Muwaza kwa heshima zote. Ingekuwa vyema ukatufahamisha hasara gani itapatikana ikiwa Rais wetu atahudhuria Baraza la Mawaziri la Jamhuri . Rais wa ZNZ ni muhimili wa Union , jee kuna ubaya gani kikatiba kuchukuwa kiapo cha Utii katika kutumikia Muungano ?
    Ilivyokuwa una ujuzi mkubwa wa mambo haya ,tafadhali tufahamishe ili tuwatahadharishe viongozi na Wananchi wa ZNZ juu ya hasara itakayopatikana ikiwa Rais atahudhuria Baraza la Mawaziri na kutii kiapo cha kuwa muaminifu kwa Jamhuri .Sisi ni Wa ZNZ ambao ni Raia wa Tanzania tunatumia Passport ya Tanzania .

    Pia tueleze hasara itakayopatikana kwenye Afya,Elimu,Kilimo, Haki ya Binadamu,Ustawi wa Jamii,Ajira , Mishahara ya Wa ZNZ n.k

    ReplyDelete
  5. Mdau, nakuunga mkono kwa asilimia zote kwa comment zako! Inasikitisha sana kuona Waznz badala ya kushughulikia matatizo yetu, ya msingi tumetumbwikia ktk dimbwi la ushabik wa kijinga! Baadhi ya watu wamefikia hata kuamini kwamba matatizo yote ya ZNZ yanatokana na muungano! huku wakisahau kua hata yale yaliyo chini ya mamlaka yetu yanatushinda! Mm nilikua najiuliza hivi kuna madhara gani yanayopatikana kwa rais wa znz kula kiapo kile?

    ReplyDelete
  6. Napenda kuchukua fursa hii kuungana na baadhi ya wachangiaji wengine hapo kwamba ni muhimu kwa Rais wetu wa zanzibar kuingia katika kikao hiki kikubwa cha kimaamuzi kwa mambo yanayohusu pamoja na masuala mengine yale ya Muungano ambapo yeye ni sehemu ya mhimili huo. Ni vema tungejiuliza kwanini baadhi ya viongozi wetu tuliwachagua huko nyuma walikuwa hawafuati jambo na kuifanya Zanzibar isishiriki kikamilifu kwenye maamuzi. Ukiangalia ibara ya 33(3) ya JMT imeeleza vizuri kuwa Rais wa Muungano ndiye pia atakaye shughulikia masuala ya Tanzania Bara na Rais huyo wa Muungano hatokuwa na mamlaka ya moja kwa moja ya ndani ya Zanzibar, kwa maana hapa ni kwamba masuala yote ya ndani ya Zanzibar (ikiwa ni sehemu ya Muungano) yatakuwa katika mamlaka kamili na halali ya SMZ. Hii inatafsiri wazi kabisa kuwa Rais wa Zanzibar si msaidizi wa Rais wa JMT na ndiyo maana basi hata kama RAis wa JMT hayupo kikao cha cabinet hakiwezi kuendeshwa na Rais wa Zanzibar (ibara ya 54(2). Rais wa JMT hana mamlaka ya kudelegate kazi kwa Rais wa SMZ kwa mujibu wa katiba. Ningeona vibaya sana kama katiba ingemuweka Rais wa Zanzibar au kumpa uhalaliwa wa kuwa msaidizi wa Rais ya JMT. Kwa maana hiyo basi heshima na hadhi ya Zanzibar haikupokwa kama mtoa mada anavyofikiria.
    Lakini jambo jengine la msingi ni kwamba tuangalie faida na hasara za Rais wetu kuhudhuria au kutohudhuria. Endapo sisi wanzanzibari tuna wabunge katika bunge la JMT, iweje Rais wetu asihudhurie cabinet? Kuendesha nchi kunahitaji kupata taarifa na kutoa maamuzi sahihi kwa nini tumtenge Rais na masuala yanayohusu maamuzi ya kimuungano? Ninaziona faida nyingi sana za Rais kufanya maamuzi ya kuingia kwenye cabinet kwani hatakuwa kiongozi wa kuletewa taarifa tu kwa yale yaliyoamuliwa kwenye cabinet bali ataweza kushiriki kikamilifu kufikia maamuzi kwa manufaa ya nchi yetu na Muungano pia.

    ReplyDelete
  7. Ah....MUWAZA, wazeni mambo ya maana..acheni ushabiki!

    ReplyDelete
  8. Ama, Dr. wetu ameshikwa pabaya! sijui ni PhD holder au ni medical doctor huyu? kazi... kweli-kweli!!!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.