Habari za Punde

AJALI ZA BARABARANI NI KICHOCHEO CHA UMASIKINI KATIKA JAMII

Na Nafisa Madai-Maelezo

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Kitaifa ya Usalama Barabarani Zanzibar Abdallah Mwinyi Khamis amesema athari mbaya zinazosababishwa na ajali za barabarani zimekuwa kichocheo kikubwa cha kusababisha umasikini katika jamii.

Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na Maazimisho ya Muongo wa Miaka Kumi wa Usalama Barabarani huko ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar


Amesema lengo la Mpango huo ni kuhakikisha Zanzibar inapunguza idadi ya vifo vinavyosababishwa na ajali za barabarabani kwa kiasi cha Asilimia 50.

Abdallah Mwinyi amesema Zanzibar inaunga mkono Azimio hilo la Umoja wa Mataifa katika kupambana na vifo vinavyosababishwa na ajali za barabarani na kwamba kama litatekelezwa ipasvyo wodi za majeruhi wa ajali za barabarani na vitanda vyake katika Hospitali za Zanzibar zitabaki tupu.

Aidha Mwenyekitia huyo amesema kiasi cha vifo vya watu milioni 1.3 na majeruhi Milion 50 hutokezea kila mwaka duniani ambapo amesema vifo hivyo ni vingi ikilinganishwa na Vifo vinavyosababishwa na Maleria na Kifua kikuu.

“Katika kuhakikisha mpango huo unafanikiwa Zanzibar,kamati ya Usalama barabarani itatumia mbinu kama zilizozitumika katika kupambana na Malaria ili Zanzibar nayo iwe ya kupigiwa mfano si tu kwa Malaria lakini pia kwa ajali za barabarani” Alisema Abadallah Mwinyi

Miongoni mwa mikakati ambayo inatarajiwa kuchukuliwa na Kamati hiyo Mwenyekiti huyo amesema ni pamoja na kuwajengea uwezo watendaji katika taasisi husika na kushajihisha utengenezaji wa baraba zilizo salama kwa watumiaji.

Mikakati mingine ni pamoja na kushajihisha uundaji magari yanayozingatia usalama wa uwendeshaji na watumiaji wengine wa barabara pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma baada ya ajali.

Uzinduzi wa Muongo wa Miaka Kumi unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Disemba 14 na Rais wa Zanzibar Dk. Shein katika Ukumbi wa Salama Holi Bwawani ambapo mbali na uzinduzi huo Rais ataongoza matembezi kutoka Hoteli ya Bawani mpaka Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa kutembelea wagonjwa waliopata ajali.


Mpango huo unaojulikana kama Decade of Action umeasisiwa katika Mkutanio wa Umoja wa Mataifa na kupitishwa kwa azimio lake Machi 3, 2010 baada ya kuwasilishwa katika Mkutamo huo na mataifa mawili kwa pamoja ambayo ni Oman na Urusi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.