Na Khamisuu Abdallah
CHAMA cha Walimu Zanzibar (ZATU) kinatarajia kuadhimisha miaka kumi toka kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 2002.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, ofisini kwake kijangwani, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Salim Ali Salim alisema ZATU imeamua kufanya madhimisho hayo kwa lengo la kukitangaza chama chao pamoja na kazi wanazozifanya ili kuweza kutambulika zaidi katika jamii.
Alisema sherehe hizo zinatarajiwa kuanza Februari 4 hadi 14 Febuari mwakani maadhimisho ambayo yatahusisha usafi katika jengo la ofisi ya chama cha ZATU kilichopo Pemba na kwa Unguja watasafisha maeneo ya Tunguu ambapo wanatarajia kujenga ofisi ya ZATU, pamoja na jukwaa la walimu vijana litakalofanyika katika mkoa wa kusini Pemba.
Aidha alifahamisha kuwa sherehe hizo pia zinatarajiwa kufanyika kwa matembezi maalum kwa walimu kama ni ishara ya kusherehekea miaka kumi ya kuanzishwa chama hicho.
"Siku ya Februari 11 pia tutakuwa na matembezi maalum kwa walimu na wanachama wetu kama ni ishara tosha ya kusherehekea miaka kumi ya chama chetu" alisema Salim.
Salim alisema kuwa katika kilele cha kutimiza miaka 10 wanatarajia kuzindua kitabu ambacho kitaonesha kazi zote zilizofanywa na chama chao kwa muda wa miaka 9
"Pia siku ya kilele cha 10 tunatarajia kuzindua kitabu ambacho kitaonesha kazi zote zilizofanywa na chama chetu kwa muda wa miaka 9 iliyopita lakini hadi hivi sasa hatujajua kitabu hicho kitakuwa na jina gani" alisema Naibu huyo.
Kongamano la kutimiza miaka 10 ya chama cha walimu Zanzibar (ZATU) linatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa serikali.
No comments:
Post a Comment