Habari za Punde

Balozi Seif akutana na Mwakilishi wa Teknolojia ya Afya .kutoka Marekani

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Mwakilishi wa Taasisi inayojihusisha na  huduma za Teknolojia ya Afya Nchini Marekani ya Med International Bwana Jayson Marwaha ambaye wapo Nchini kufanya utafiti wa Afya kwa Hospitali za Zanzibar. Hatua hii ni utekelezaji wa ahadi waliyompa Balozi Seif wakati walipokutana nao Nchini Marekani Mwezi Oktoba Mwaka jana.
Kushoto ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Dr. Sira Ubwa Mwamboya.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Mwakilishi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi inayojihusisha na huduma za Teknolojia ya Afya ya Chuo Kikuu cha Brown Mjini Boston Nchini Marekani Bw. Jayson Marwaha hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Kati kati ni Mkurugenzi Mwenza wa Taasisi hiyo ya Med Intarenational Bwana Han Sheng Chia.
Picha na Saleh Masoud OMPR
Na Othman Khamis Ame

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kupokea Msaada wa Mashine za Uchunguzi wa Damu { DNA } wakati wowote kuanzia Mwezi wa Julai Mwaka huu kutoka Taasisi inayoshughulikia Taaluma ya Teknolojia ya Afya ya Chuo Kikuu cha Brown Mjini Boston Nchini Marekani { MED International }.

Msaada huo unafuatia ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyoifanya Mwezi wa Oktoba Mwaka uliopita Nchini Marekani ambapo alipata fursa ya kufanya kwa mazungumzo na Uongozi wa juu wa Taasisi hiyo.

Mwakilishi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi hiyo ya MED International Bwana Jayson Marwaha alieleza hayo wakati alipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Jayson akiwa na Mkurugenzi mwenza wa Taasisi hiyo Bwana Han Sheng Chia amemueleza Balozi Seif kwamba sambamba na Msaada huo wamekuja Zanzibar kufanya Utafiti wa Afya katika Hospitali tofauti za Serikali za Unguja na Pemba.

 “ Lengo letu la kufanya Utafiti huo hapa Zanzibar ni kuangalia maeneo na vifaa gani vinahitajika na tutakaporejea kwenye Taasisi yetu tuweze kuyachukulia hatua kwa nia ya kuimarisha Ustawi wa Jamii hasa ile ya kawaida”. Alifafanua Mkurugenzi huyo wa MED International.

Bwana Jayson alieleza kwamba katika kuona Taaluma ya kiuhandisi ndani ya Sekta ya Afya inakuwa Kiteknolojia Taasisi yake inatarajia pia kuleta Mabingwa wa fani hiyo mnamo Mwezi wa Agosti Mwaka huu.

Katika Mazungumzo yao Nchini Marekani Mwaka jana Bwana Jayson aliwahi kumuahidi Balozi Seif kwamba Taasisi yake itaandaa taratibu kwa Wataalamu wake kufanya kazi za kujitolea Hapa Zanzibar.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Taasisi hiyo inayoshughulikia Taaluma ya Teknolojia ya Afya { MED International kwa uamuzi wake wa kusaidia huduma za Afya hapa Zanzibar.

Balozi Seif ameelezea kufarajika kwake na ujio wa Uongozi wa juu wa Taasisi hiyo ambao umeonyesha uungwana katika kutimiza ahadi zake ilizozitowa Mwaka jana Nchini Marekani.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza Ujumbe huo wa Med International kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuimarisha zaidi huduma za Afya katika Hospitali zake zote Unguja na Pemba.

Mapema Naibu waziri wa Afya Zanzibar Dr. Sira Ubwa Mwamboya alisema Ujumbe huo umekuja wakati muwafaka kwa vite bado eneo la Fani ya Sayansi katika chuo cha Sayansi ya Afya Mbweni linahitajika. Ujumbe huo wa MED International tayari umeanza kukutana na washirika wao wa Sekta ya Afya hapa Zanzibar katika kujiandaa na Taratibu za kuanza Utafiti huo unaotarajiwa kuendelea hadi Septemba 2 Mwaka huu.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amekabidhi msaada wa gari moja kwa ajili ya matumizi ya shughuli za Jumuiya ya Fiy Sabilillah Markaz ya Fuoni. Balozi Seif alisema ameamua yeye binafsi kupitia wafadhili pamoja na Familia yake kutoa msaada huo kutokana na mchango mkubwa unaotolewa na Jumuiya hiyo ndani katika kueneza Daawa kwa Jamii.

Balozi Seif ameipongeza Jumuiya hiyo kwa kutojiingiza katika masuala ya Kisiasa na kuahidi kutoa mchango wa Shilingi 500,000/- kusaidia harakati za Taasisi hiyo. Mapema katibu wa Jumuiya ya Fiy Sabilillah Markaz ya Fuoni Sheikh Mwalimu Hafidh Jabu ameuomba Uongozi wa Serikali kuwa karibu zaidi na Jumuiya hiyo kwa lengo la kufanikisha majukumu waliyojipangia.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Sheikh Ali Khamis amesema kitendo cha Serikali Kupitia Wizara ya Miundo Mbinu na Mawasiliano kuifanyia matengenezo Bara bara ya Fuoni hadi Markaz kinafaa kupongezwa na kushukuriwa.

Sheikh Ali alisema bara bara hiyo hivi sasa imeleta faraja kwao na hata kwa Wananchi wa Eneo la Fuoni ambao kwa kipindi kirefu walikuwa wakikabiliwa na Tatizo sugu la ubovu wa Bara bara hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.