Habari za Punde

Waziri Masoud Amuonya Afisa wa Mamlaka ya Usafiri Bandari ya Mkoani

Na Nafisa Madai-Maelezo.
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Hamad Masoud Hamad amemuonya Afisa wa Mamlaka ya usafiri wa Baharini ZMA Khamis Bakari kwa kuzembea katika kazi yake.
Onyo hilo alilitoa jana katika bandari ya Mkoani baada ya Khamis kutokuwepo Bandarini hapo na hivyo kushindwa kutimiza wajibu wake wa kuhakiki idadi ya abiria waliokuwa wakishuka katika boti ya See buss 1.

kutokana na hali hiyo ya kutokuwepo afisa huyo Waziri Masoud alilazimika kuhesabu abiria wa boti hiyo ili kujua idadi ya abiria kulingana na uwezo wa boti uliopangwa kwa mujibu wa taratibu.
Waziri Masoud alipokutana na Afisa huyo ambaye tokea aajiriwe ana mwaka mmoja alitaka kujua sababu ya kukosekana Bandarini hapo ambapo Afisa huyo alidai kuwa alienda kujisaidia haja ndogo.
Aidha alimtaka afisa huyo kutodharau kazi yake ili kuepuka majanga ya ajali za baharini ambayo kamwe Serikali haitoweza kuyavumilia.
Waziri Masoud alisema Serikali kupitia wizara yake ipo makini sana na haitokuwa na huruma kwa mtu yeyote atakaezembea katika kazi zake hasa ambazo huhatarisha maisha ya watu wengi.
Amefahamisha kuwa lengo la kuwepo kwa Maafisa wa ZMA katika bandari zote ni kuhakikisha abiria waliomo ndani ya chombo wanaendana na idadi halali ya chombo walichopanda.
Alisisitiza kuwa uzembe uliofanyika wakati wa ajali ya Mv Spice wa kutokujua idadi sahihi ya abiria walikuwemo katika meli hiyo hautakiwi kutokea tena na kwamba maafisa hao wanatakiwa kufanya kazi kwa uhakika na sio kubahatisha.
Boti hiyo ya See bus 1 iliondoka unguja saa moja asubuhi ikiwa na abiria 197 watu wazima,watoto 30 na wageni 2 (wazungu) na kufika katika gati mkoani saa 5 asubuhi ikiwa katika hali ya kawaida.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.