Assalamu'alaykum Warahmatu Llahi Wabarakatuh,
Shukrani zote ni zake Muumba wa mbingu na aradhina,
Muumba aliyezitukuza siku chache za mgeni wetu Ramadhaan kwa kujaaliya mambo mengi ndani yake, Muumba aliyemtunuku
Ramadhaan zawadi tukufu ya kuwa ndio
wakati aliouchagua wa kuyaleta/kuyashusha maneno yake matukufu, ambayo ni
uongozi na uongofu kwa viumbe wote, Qur-an
inasema:
“Mwezi
wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja
zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi..” Al-Baqarah aya ya
185.
Rehma na Amani za Allah zimfikie Al-Habibi
Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa'ala Alihi Wasallam) na kila
aliyejaaliwa kufuata na kushikamana na mafunzo yake sahihah,
yeye al-Habibu Musttafa (Salla Allahu 'Alayhi Wa’ala Alihi Wasallam)
amepokelewa –Hadithi Qudsy- akisema
kuwa: Allah amesema:
“Kila ‘amali anayoifanya mwanadam huengezewa, jema moja kwa kumi mpaka
mia saba, na halafu huengezwa kwa atakavyo Allah,
isipokuwa sawm (funga), hiyo (sawm/funga) ni Yangu Mimi, na Mimi ndiye
Mlipaji wake ….” Imepokelewa na Muslim, kitabu cha sawm, mlango
wa fadhila za sawm.
Ndugu zangu wapenzi katika imani, napenda kujiusia
nafsi yangu kwanza na nasfi zenu kumcha Allah na kumtii,
kwa kutekeleza kila aliloliamrisha kadiri ya uwezo wetu, na
kujikataza na kila alichokikataza mara moja.
Ndugu zangu katika imani,
Ramadhaan ni mgeni aliyejenga
uhusiano mzuri na wenye nguvu na Waislamu wa kila zama, kwa njia ya
kuwatembelea katika nyumba zao kwa kukaa na kuiishi nao kwa wakati wote wa
kipindi cha mwezi mzima. Mgeni huyu
ndiye yule yule aliyewahi kuwatembelea na kukutana uso kwa uso mara karibu tisa
na al-Habibi Musttafa (Salla Llahu
‘Alayhi Wa’ala Alihi Wasallam), kipenzi chetu na kipenzi cha wote wenye kumtarajia
Allah na Siku ya Mwisho na
wakamkumbuka Allah sana, mgeni huyu
aliwahi pia kuwatembelea Sahaba (Radhiya Llahu ‘Anhum) na waislamu wote wa karne zilizopita, na ni
huyu huyu ataewatembelea insha Allah kwa
uwezo wake Mola waislamu wa karne zitakazokuja baada yetu tutakapokuwa chini ya
tani za udongo.
Twamuomba al Hayyu al
Qayyuum atusamehe makosa yetu na madhambi yetu makubwa na madogo, ya mwanzo
na ya mwisho, tuliyoyafanya kwa dhahiri na kwa siri, na aturuzukuku maghfirah na tawbah kabla ya kuiaga dunia
hii yenye kutushughulisha karibu wengi wetu, na tukutane naye hali ya kuwa ni
waislamu waliosamehewa na waliokubalia tawbah
zao insha Allah, Amin Amin Amin.
Ndugu zangu katika iman,
ni miongoni mwa mambo yaliyozoeleka kuwaona Waislamu wa kila nchi, miji, vijiji
na mitaa kujiwekea wakati wa kukumbushana na kuelezana namna ya kumpokea mgeni
huyu mtukufu kama ni matayarisho na mapokezi
yake. Hivyo utaona kwa mfano mihadhara kama sisi hapa leo kwa fadhila, rehma na uwezo wa Jabbaar tumekutana kwa hilo, au maandishi kwa wenye kutumia mtandao
yenye kubeba anuani kama zifuatazo:
Namna ya
kuikaribisha Ramadhaan
Vipi Tuikaribishe
Ramdhan
Mambo ya
kuikaribisha Ramadhaan
Njia kumi za
kuukaribisha vizuri Ramadhaan
Ndugu zangu katika iman, yote
haya na mengine kama haya huwa na lengo la
kuwataka waislamu kujiandaa na kujitayarisha kwa kujiweka tayari kumpokea mgeni
wao mtukufu kwa namna au njia inayokubaliwa na Allah na Mtume wake (Salla Llahu 'Alayhi Wa'ala Alihi
Wasallam).
Ndugu zangu katika imani,
matayarisho ya kumpokea mgeni ni ya namna nyingi, hasa hasa kwa kuwa mgeni
wenyewe ni ‘adhimu na ni mwenye
ku’adhimishwa na kila mwenye kuamini Allah
na Siku ya Mwisho, kwani wao pekee ndio waliotajwa na kuainishwa katika Qur-an, kuwa wamependekezewa mgeni afikie
makwao, wakae nae na kuishi nae kwa kuchunga na kuhifadhi mipaka yake,
wametajwa na kuainishwa kwa jina au sifa wanayoipenda wanasibishwe nayo bali
ndio identity yao katika uhai wao
huu na ujao insha Allah,
kinachojitokeza hapa ni vipi sisi
tutamkaribisha/tumkaribishe Mgeni huyu, mgeni ambae wenyeji wake ni watu
maalum, kama inavyothibitisha Qur-an,
Allah anasema:
“Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo andikiwa walio
kuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu “ al-Baqarah aya ya
183,
Ndugu zangu katika imani,
muhadhara wenye anuani kama hii huwa na lengo la kutupelekea kuwa na hamu na
shauku ya kujiweka tayari kwa tawfiq na
uwezo wa Mola wa Ramadhaan kumpokea
mgeni, lakini kwa kuwa wenyeji wake ni wale wenyekupenda kunasibishwa na sifa
au kuainishwa kwa jina maalum (walioamini),
jambo hili hupelekea tukawa na makundi ya watu yenye fikra na mawazo tofauti
katika kumpokea mgeni Ramadhaan,
hivyo kuwasili kwake kunawagawa waislamu (sio
waumini) katika makundi mengi yakiwemo yafuatayo:
1) Wanaompokea
mgeni kwa moyo uliojaa furaha kwa kuwa Allah
amewapendekezea mgeni na akawafiqisha kuweza kukutana na mgeni wao Ramadhaan baada ya wengi miongoni mwao
kuiaga dunia.
2) Wanaompokea
mgeni kwa manung’uniko na masikitiko kwa kuwa mgeni huyu atawanyima starehe zao
na atapekelea baadhi ya matamanio yao kutopatikanwa, bali ni maudhi na mateso
tu hakuna jipya, kwanini watu wafunge/tufunge na kujizuilia kula na kunywa! Bali hata hufikia kusema kuwa hivyo kweli Allah ameipendekeza Sawm kwa watu, jambo ambalo linapelekea kuingiliana katika mambo
binafsi na uhuru na matakwa ya mtu.
3) Wanaompokea
mgeni kwa michezo na kila lenye kupoteza wakati, (kupitisha masaa) kwao wao
kuja kwa Ramadhaan ni jambo la
kawaida na ni katika mila na desturi za jamii wanazoishi, lililo muhimu kwao ni
kuonekanwa umefunga (huli, hunywi, waweza kufanya uyatakayo kama kawaida yako
jihadhari asikuonwe na maustadhi na wapika majungu) hakuna jipya isipokuwa
kushinda na njaa, kwani majumba mengi huwa hawapiki, kwa ufupi ni mwezi wa
kushinda na njaa.
4) Wanaompokea mgeni kwa wasi wasi na shaka,
huku wakijaribu kujitetea na kutaka kuonekanwa kuwa moderate, kwani wanachokifanya
(funga) si jambo geni, wala hakuna tofauti na wengine, kwa kuwa linafanywa pia
na wengine wenye dini (Manasara, Mayahudu, na kila mwenye kujidai kuwa ana siku
katika dini yake za kufunga), hivyo hakuna jipya.
Je mimi na wewe
tumo katika kundi lipi? Tujipime kulingana na Ramadhaan tulizokutana nazo na yakaribu kabisa ni ya mwaka
jana. Je mwaka huu mgeni ndio huyo yuko
kizingitini, tunapenda tuwemo au kuingia/kujiingiza katika kundi lipi? Lenye
kupenda kunasibishwa na jina la waliotakiwa waishughulikie Ramadha kwa kuchunga, kuheshimu na kuhifadhi mipaka yake
kulingana na mafundisho ya al-Habibi Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa'ala Alihi Wasallam) au makundi yasiyopenda kuainishwa na kunasibishwa na
jina/sifa waliyonasibishwa nayo waliopendekezewa Ramadhaan?
Ndugu
zangu katika imani, mgeni yo yote
yule utaelewa hadhi yake na umuhimu wake kwa mwenyeji/wenyeji wake kutokana na
matayarisho/maandalizi na mapokezi yake, ndio sisi tukawa na anuani kama hii Vipi tumkaribishe Ramadhaan, na ili
tuelewa namna gani anahitaji kupokewa na kukaribishwa huyo mgeni wetu Ramadhaan, ni vyema kwanza
umuelewe/tumuelewe Ramadhaan wenyewe
ni nani? na baada ya hapo ndio upange, wewe na sio mimi, namna ya kumpokea na
kumkaribisha, kwani si jambo la kawaida kuwa mgeni wako na atakuwa nyumbani
kwako, bali atakuwa na wewe muda wa mwezi mzima katika masaa ishirini na nne
(24) yako ya kila siku yako, aje atokea mtu mwengine nje, akupangie namna ya
kumkaribisha!, labda awe mtu wako wa karibu sana kama vile rafiki/shoga yako na
kadhalika.
Ndugu
zangu katika imani, hata hivyo sisi
leo hapa tuko katika kukushauri/kushauriana kuwaidhiana kupeana fikra na mawazo
kupendekezeana juu ya jinsi ya kumkaribisha Ramadhaan,
na mwisho wa hayo wewe ndie muamuzi wa mwisho, hivyo suala ni hili, unamuelewa vyema mgeni wako? Kama kweli unamuelewa, basi vipi umepanga kumpokea? kama
umejipangia, na kama bado, je uko tayari kusikiliza mapendekezo yangu?
Mapendekezo ambayo kwa kweli hayana uzuri wo wote kuliko yale utakayojiwekea
wewe mwenyewe kwa hiari yako.
Ndugu
zangu katika imani, Ramadhaan au
mgeni wako (wetu) mpenzi yuko hivi kama alivyoelezwa na Mola wake, Allah anasema:
“Mwezi wa Ramadhaan ambao
imeteremshwa humo Qur-aan kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za
uongofu na upambanuzi. Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu na afunge. Na
mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine.
Mwenyezi Mungu Anakutakieni yaliyo mepesi wala Hakutakieni yaliyo mazito, na
mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa Amekuongoeni ili
mpate kushukuru” Al-Baqarah:
aya ya 185, pia al-Habibu Musttafa (Salla
Allahu 'Alayhi Wa’ala Alihi Wasallam) amesema:
“Mwenye kufunga Ramadhaan (kama inavyotakiwa na sio
kukaa na njaa) kwa iman
na kutaraji malipo, atasamehewa
madhambi yake yote yaliyotangulia” Imepokelewa na Bukhar,
kitabu cha saum, mlango wa mwenye kufunga Ramadhaan
kwa iman, pia al-Habibu Musttafa (Salla Allahu 'Alayhi Wa’ala Alihi Wasallam) amesema:
"Inapoingia Ramadhaan, milango ya Pepo hufunguliwa
na milango ya Moto hufungwa, na mashetani hufungwa …" Imepokelewa na Muslim, kitabu cha saum, mlango wa
fadhila za mwezi wa Ramadhaan,
Ndugu
zangu katika imani, miongoni mwa mambo yanayotupelekea kuwa na mihadhara kama
hii itakayoweza kwa tawfiq ya Mola
kutupelekea kujiandaa vizuri, ni ile hadithi iliyothibiti ya al-Habibi Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa'ala Alihi Wasallam) kuwa alisikiwa akisema Amin
Amin Amin mara
tatu (3) huku alipanda minbar, alipomaliza Sahaba (Radhiya Llahu ‘Anhum) walimuuliza kwa mshangao mkubwa, mbona
umeitikia Amin Amin Amin, mara tatu huku ukipanda vidaraja vya minbar, jambo ambalo si kawaida yako,
hukuomba dua, je kuna liilojiri?! al-Habibi Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa'ala
Alihi Wasallam) aliwajibu
kwa kusema:
“Amenijia Jibril –‘Alayhis Slaam-
na kuniambia kuwa: yuko mbali na Rehma
za Allah yule
ambae ametembelewa na Ramadhaan
na akashindwa kutekeleza kitachopelekea kufutiwa madhambi yake, -nilinyamaza
kimya, Jibril
akanitaka niitikie kwa kusema: Amin, nikasema: Amin
-akaendelea kusema:yuko mbali na Rehma za
Allah yule
ambae atasikia jina lako linatajwa, na akawa hana nafasi ya kukusalia,
-nilinyamaza kimya, Jibril
akanitaka niitikie kwa kusema: Amin,
nikasema: Amin-,akaendelea
kusema: kuwa yuko mbali na Rehma za Allah
yule ambae amejaaliwa kuwakuta wazazi wake wawili na akashindwa kuingia
peponi!, -nilinyamaza kimya, Jibril akanitaka
niitikie kwa kusema Amin
nikasema Amin”
Ndugu
zangu katika imani, tujaribu kuwa na
tabia ya kujiwekea mipango, malengo, njia na mbinu za kutekeleza mambo yetu,
njia za kujitayarisha katika kuyatekeleza na kadhalika, tena tuwe wakweli na
wawazi katika mipango yetu, kwa mfano na haya
ndio hasa tunayoyapendekeza na kuyataka tuwe nayo katika kumpokea mgeni:
Azimia kuwa mgeni
utampokea kwa kila aina ya ‘amali njema
na utajitahidi kiasi cha kumthibitishia mgeni kuwa katika wageni wako wote
wanaokutembelea nyumbani kwako na kuishi na wewe ni yeye Ramadhaan ndiye unaempenda na kumthamini, kwa sababu kubwa moja, ni
mgeni aliyependekezwa na Mlinzi wa Waumini ni Mlinzi Mwema na Msaidizi Mwema, kuwa awe mgeni wako ili kwa tawfiq yake upate yale aliyoyaandaa na kuyatunuku ndani yake.
Tafadhali angalia nini uliwafiqishwa mwaka jana na kile ulichoshindwa
kukitekeleza ukiwekee mikakati ya kukitekeleza mwaka huu, azimia kuwa mwezi
wako huu uwe ndio mwezi bora utaoishi nao na kutekeleza utachojaaliwa na
kuwafiqishwa kutekeleza ukijilinganisha na miezi yote iliyopita ikiwemo Ramadhaan yako ya mwaka jana.
Weka mikakati na
mipango yenye uhakika itakayo kupelekea kuweza kuitekeleza tena kwa ufanisi na
bila uzito, wakati wote mgeni akiwa na wewe; kwa mfano:
Fufuwa au imarisha
uhusiano wako na Mola wa Ramadhaan, kwa
kumsikiliza na kumuitika, kwa kujizowesha kuwa karibu na maneno yake ambayo
aliyachagulia mwezi wa Ramadhaan kuwa
ndio wakati wa kuyateremsha. Jipangie wakati maalumu wa kuzungumza na As Samiy’ul Bassiyr, shauriana na ahli zako, rafiki zako, jirani,
mnaofanya kazi pamoja, mnaocheza mpira pamoja, au wenzako mnaosali pamoja,
shauriana nao kuchagua wakati na pahala muwafaqa pasipohitaji taklifah, ambapo mutaweza kwa tawfiq yake Mola kukaa pamoja na
kuzungumza na Rahmaan, kwa mfano: kila baada ya sala fulani, nyumbani
kwa fulani au msikiti fulani au klabu fulani.
Pia jiwekeeni wakati wa kuhifadhi maneno yake matukufu na kusikilizana hifdh yenu, jipangieni wakati wa
kujielimisha na kuweza kufahamu maana yake, ili uweze kwa tawfiq yake Mola wa Ramadhaan
kujiengezea na kujizidishia iman yenu
na yaqini itakayo
kupelekea/kupelekeeni kuweza kutekeleza maamrisho yake na kuwacha makatazo yake
kama atakavyo Al-Wahiyd al Qahhar.
Fufuwa au imarisha
uhusiano wako na sala tano, tumia
diplomasia yako katika kisimamo chako cha sala tano kiijumuishe mahusiano na
sala za usiku, fufuwa, imarisha sala zako kwa kuzipa uhai mpya, jaribu
kurefusha visimamo, rukuu na sijdah za sala zako, fufuwa, imarisha au huisha
sala za sunnah zote zikiwemo zile za
kabla hujalala witr au kabla salatul fajiri au zile za usiku tahjjud.
Imarisha uhusiano
wako na jamaa zako, kwa kuwatembelea
wazee wako au kuwasiliana nao, pia kwa kuwapa au kuwatengea sehemu katika kile
alichokuruzuku Mola wa Ramadhaan
kabla hujaiaga dunia.
Imarisha, fufuwa
au anza kujifunza namna ya kuthamini wakati wako, chunga wakati wako katika
shindano hili kubwa la mwaka lenye kushirikisha kila mwenye kuamini Allah na Siku ya mwisho. Imarisha,
fufuwa au jizoeshe na uzoeshe ulimu wako na moyo wako na ahli zako na wenzako katika baraza zako kumkumbuka na kumtaja kwa
wingi Mola wa Ramadhaan na
kumsalia/kumtakia Rehmah na Amani al-Habibi Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa'ala Alihi Wasallam) aliyetufunza yote
tunayoyahitaji katika uhai huu, yakiwemo tunayohitajia tuyafanye na kuyaomba
wakati mgeni akiwa katika nyumba zetu, alikuwa al-Habibi Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa'ala
Alihi Wasallam ) yakimhuzunisha sana
yanayo tutaabisha; aliyekuwa akituhangaikia sana na kwa waliopendekezewa mgeni
mtukufu.-Waumini- alikuwa al-Habibi
Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa'ala Alihi Wasallam) ni mpole na mwenye huruma sana, kama ilivyothibisha hayo Qur-an
tukufu, Allah anasema:
“Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na
nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na
mwenye huruma “ at-Tawbah aya ya 128.
Imarisha,
fufuwa au anzisha uhusiano mkubwa na wenye nguvu wa kumuomba mwenye kupenda
kuombwa na aliyekupendekezea namna ya kumuomba, Allah anasema:
“Na Allah ana
majina mazuri kabisa, basi muombeni kwa hayo… “al-A’raaf aya ya 180; na wakati wa
kumuomba pia, Allah anasema:
“Na waja wangu
watakapo kuuliza khabari zangu, waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi
ya mwombaji anapo niomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili
wapate kuongoka “ al-Baqarah aya ya 186; pia al-Habibi Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa'ala
Alihi Wasallam) katika
kutuhangaikia ametupendekezea wakati wa kupeleke maombi yenu kwa kusema:
“Allah anashuka katika
mbingu za dunia kila usiku katika thuluthi ya mwisho na
kusema; "Yuko mwenye kuniomba nimkubalie maombi yake?, Nani aniulizae
nimpe?, Nani aniombae msamaha (Maghfirah)
nimsamehe?." Imepokelewa na Bukhar, milango ya Tahajjud
(kisimamo cha usiku), mlango wa dua na sala katika sehemu ya mwisho wa usiku.
Ndugu
yangu katika iman, huisha na sisitiza kumtaka na kumuomba msamaha kwani
Yeye ni Ghaffar, sisitiza kumuomba rehma zake kwani Yeye ni Arhamur Raahimiyn, sisitiza na shikilia
kumuomba akuepusha na akute katika moto kwani Yeye ni Qaadir wa kila kitu na ni Mwenye kufanya alitakalo na wewe ni mja wake
dhalili, muhitaji na ni mwenye kukiri madhambi na taqssiyr .zako, na
Yeye ni Msamehevu na Mwenye Rehma, Qur-an inasema:
“Na wengine walikiri dhambi
zao, wakachanganya vitendo vyema na vingine viovu. Asaa Allah akapokea toba
zao. Hakika Allah ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu “ at-Tawbah aya ya 102.
Imarisha, fufuwa au huisha darasa yako, kama hakuna, basi pendekeza na
shajiisha kuwepo kwa darasa, mihadhara, kufutarishana, kuwaidhiana, kukutana
kwa ajili ya Allah, ambapo wewe na ahli zako utakuwa muhusika wa kwanza, mhudhuriaji wake na
mtangazaji wake, na mhakikishaji kuwa haitapata pingamizi ya aina yo yote ile
katika kuwepo kwake, iwe pingamizi ya pahala au malipo ya pahala, au hata
vifuturishaji kama vitahitajika.
Darsa/mawaidha na mikusanyiko kama hii yenye kutajwa Allah na Mtume wake al-Habibi Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa'ala
Alihi Wasallam) na waja wema ni pahala patakapo
kupelekea kuwa karibu na Allah, kwani
ni pahala unapokumbushwa na kushajiishwa kila lenye kukupelekea kuweza kwa tawfiq yake Mola kukufikisha kwenye
lengo kuu lililosababisha Ramadhaan ipendekezwe
na Mola wake kuwa iwe mgeni wako katika masiku yake machache na matukufu, na hayo ni miongoni mwa vyakula unavyovitajia, vyakula vya moyo wako,
mwili wako unahitaji vyakula vya namna mbili; kimoja cha kukuza mwili na
chengine cha kukuza iman yako ambacho
utakipata tu ukiwa karibu na wenye kupenda kunasibishwa na imaan.
Fufuwa, imarisha au anzisha uhusiano wa kuwalingania watu kwa hikmah na mawaidha mema na mazuri kabisa
na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora na
iliyozuri zaidi, kama inavyotupendekezea Qur-ani, Allah anasema:
“Waite
waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na
ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua
zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka. “an
Nahl aya ya 125, tumia diplomasia
yako katika da’wah, wewe uko tayari
kumkinaisha kila mtu kwa ulitakalo, kwa nini usitumie uwezo wako huo aliokupa
Mola wa Ramadhaan kuwakinaisha
angalau Ahli zako, jamaa zako, rafiki
zako, waswahili wenzako, kufikia kutekeleza maarisho ya Mola wako na hasa
yatakayowapelekea kunufaika na kufaidika na Ramadhaan
ambayo unaielewa vyema umuhimu wake katika maisha yako ya hapa duniani na kesho
Akhea utakapokuwa chini ya udongo.
Orodhesha a’maali njema ambazo
utapenda kwa tawfiq ya Mola wa Ramadhaan uzitekeleze katika mwezi huu,
kwa mfano jipangie na jiwekee kusoma kitabu fulani; katika ‘aqidah – ‘aqida ya Twahaawiyyah-,
katika sala – Sala kama alivyoisali al-Habibi Musttafa (Salla
Llahu 'Alayhi Wa'ala Alihi Wasallam), Sawm na kadhalika.
Ndugu zangu katika iman, haya
yote yanawezekana, na wewe na mimi tutayaweza kama tutaamuwa na kuchukuwa hatua
moja muhimu; kabla ya kuichukuwa hatua hiyo, ni vyema tuelewe (mimi na wewe
wenye kutaka kununuwa bidhaa ya Allah),
ni vyema tuelewe kuwa bidhaa tuitakayo imezungukwa na kila lisilo pendwa na
kuvutiwa na nyoyo zetu, na moto ambao hufungwa milango yake katika mwezi huu,
umezungukwa na kila linalo pendwa na kufurahiwa na nyoyo na nafsi zetu; hivyo
basi simamisha bali vunja mawasiliano na uhusiano wako mzuri na wenye nguvu na
wa karibu sana na shayttaan, mwenye
nafasi kubwa na ya pekee katika kila nyumba, tuliyemnunuwa kwa fedha
alizoturuzuku Mola wa Ramadhaan, TV; chakufanya au mapendekezo:Itumie kwa
kuangalia yatakayo kuletea kheri kama kuangalia mihadhara, mawaidha, iwe ndani
ya mwezi wa Ramadgan au miezi mengine
kama huwezi kumkosa. Jaribu kumsilimisha Shayttaan
wako ili ufaidike na ugeni wa Ramadhaan
katika nyumba yako.
.
Ndugu
yangu katika iman, tukipata ushauri
kwa wenzetu ushauri ulio mzuri basi tuwe tayari kuusikiliza na kuufikiria
kuutekeleza kama tutauona unamuelekeo mzuri na wenye kushikamana na mwenendo wa
Al-Habibi
Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa'ala Alihi Wasallam) na watu wema waliotutangulia
ambao katika uhai wao walishikamana na mwenendo wa Al-Habibi
Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa'ala Alihi Wasallam) bila ya kutia mawazo au fikra
zao katika waliyoshikamana nayo.
Ndugu
zangu katika iman, tujaribu kuishi
wakati wetu huu na al-Habibi Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi
Wa'ala Alihi Wasallam) ili tuangalie vipi yeye Al-Habibi Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi
Wa'ala Alihi Wasallam) alikuwa akijitayarisha kumkaribisha na kumpokea Ramadhaan,
na vipi alikuwa
akiishi na Ramadhaan, yote haya kwa kuwa Yeye Al-Habibi
Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa'ala Alihi Wasallam) ni Ma’asuum, ambaye kwa maneno yake hupimwa
maneno, na kwa matendo yake hupimwa vitendo, na kwa hali yake husahihishwa
hali.
Ndugu
zangu katika iman, ni hakika
isiyopingika kuwa mwenye kumfuata, na kuigiza mwenendo wake, na kuongoka kwa sira yake al-Habibi Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa'ala Alihi
Wasallam) ndie mwenye kheri nyingi na insha Allah ndiye atae faulu na kufanikiwa
katika hii dunia na kesho Akhera, na ni hasara kubwa isiyopimika
na kuharibikiwa kusiko elezeka kwa yule asiye mfuata al-Habibi Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi
Wa'ala Alihi Wasallam) katika kila nyaja ya maisha yake ya kila siku hapa duniani na huko
twendako kwa uhakika.
Ndugu zangu katika iman, al--Habibu Musttafa (Salla Llahu
'Alayhi Wa’ala Alihi Wasallam) alikuwa akimpokea Ramadhaan
kwa mapokezi yaliyojaa na kila aina ya furaha na maandalizi yenye kuonyesha
na kuthibitisha kuwa mja yuko tayari kuingia kwa tawfiq ya Allah katika
masiku yanye fadhila na kila lenye kupendwa na Rahmaan, mja yu tayari kuingia katika mwezi ambao kwa tawfiq yake Rahmaan ukimalizika, awe katika walioghufuriliwa na kutolewa katika
moto wa Jahannam, mja yu tayari
kukutana na kuishi msimu wa mavuno, mavuno atayoyahitajia bila ya shaka wala
wasi wasi wa aina yo yote ile atakapokuwa chini ya udongo, mja yu tayari
kukutana na msimu wa kheri, msimu wa Rahmah,
msimu wa Maghfirah, msimu wa kutolewa
watu katika moto wa Jahannam.
Imethibiti katika hadithi kuwa al--Habibu
Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa’ala Alihi Wasallam) akiuona mwezi
muandamo wa Ramadhaan alikuwa akisema:
“Allahu Akbar, Ewe Mola Uanzishe kwetu
–mwezi muandamo- kwa aman na iman, na usalama na Uislam, na tawfiq ya kutekeleza kila
ukipendacho na ukiridhiacho, -pia alikuwa akiuthibitishia mwezi kwa kuusemeza
na kuuambia kuwa- Mola wangu na Mola wako ni Allah”. Imepokelewa na …………………….
Ndugu zangu katika iman, al--Habibu Musttafa (Salla Llahu
'Alayhi Wa’ala Alihi Wasalla) alipokuwa
akisema maneno haya (akiomba dua hii) ilikuwa Ramadhaan ndio ishaingia kwani kuandama kwa mwezi ndio kuanza
kwake, hivyo kahuwa akiukaribisha kwa hayo, kwani mwezi ushaingia, bali alikuwa
akiomba awafikishwe ndani yake kwa yale aliyoyaona ni muhimu, nasi leo
tunashauriana juu ya namna ya kuukaribisha Ramadhaan,
ningependelea mara nyengine kama tutajaaliwa kuwa hai na uzima kuelekea
kuwa na tamaa ya kukutana tena na Ramadhaan,
tuweke wiki ya mwanzo ya Shaaban kuwa
ndio wakati wa kushauriana namna ya kumpokea Ramadhaan, kwa kuwa matayarisho ya kumpokea mgeni mwenye nafasi
kubwa katika nafsi za waumini hayawezi yakawa ya siku tatu au tano kabla ya
kuwasili mgeni, hasa tukielewa kuwa bidhaa yake Mola wa Ramadhaan ambayo tunaitarajia kuinunua –kama tunacho cha kununulia-
au kutunukiwa –kama tunazosababu za kuthibitisha kuwa tunastahiki kutunukiwa-
au kuiomba - kama maombi yetu yanatimiza masharti ya kukubaliwa- tunaiomba tena
kwa wingi katika masiku haya machache, bidhaa yake Mola wa Ramadhaan si rahisi, bidhaa yake anayoiuza ni ghali sana, bidhaa
yake ni Jannah.
Kisha tujipangie
kuwa wiki ya mwisho ya Shaaban kama
leo, tuiweke au tuitumie kwa kutathmini maandalizi yetu tuliyojiwekea katika
kuikaribisha Ramadhaan na kujiandaa
kwa kukutana naye mgeni kwa kujikumbusha na kurejea sharia na hukumu za Sawm na yote yenye kufungamana na Sawm, nini cha kufanya ndani ya mwezi
mzima wa Ramadhaan na kadhalika.
Ndugu
zangu katika iman, hata hivyo
tutashauriana na kujitahidi kutekeleza tutakayowafiqishwa, kwani kila kitu ni
kwa tawfiq yake Mola wa Ramadhaan.
Ushauri au pendekezo langu ni kuwa kwa kuwa siku zilizobakia ni
chache, basi tujitayarishe na tujiandae kwa kumpokea mgeni wetu kwa mambo
yafuatayo, mambo ambayo tutajaribu kuyachukuwa kutoka kwa al--Habibu Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi
Wa’ala Alihi Wasalla) kwani kama ilivyothibitisha Qur-an kuwa yeye ndie wa kufuatwa na
kuigwa kama tunataka kuongoka na kutengenewa mambo yetu, Allah anasema:
“Hakika nyinyi mnayo
ruwaza njema kwa Mtume wa Allah kwa anaye mtaraji Allah na Siku ya Mwisho, na
akamkumbuka Allah sana“al-Ahzaab aya ya 21
Ndugu zangu katika
iman, imethibiti kuwa al--Habibu Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa’ala Alihi Wasalla) katika kujiandaa
kwake kumpokea Ramadhaan, alikuwa
akifunga sana katika mwezi wa Shaaban, mpaka
ikafika wakati Sahaba (Radhiya Allahu
‘Anhum) wakawa hawaelewi lini al--Habibu Musttafa (Salla
Llahu 'Alayhi Wa’ala Alihi Wasalla) ameamka amefunga na lini
ameamka hajafunga,:
“Mtume Salla Llahu 'Alayhi Wa’ala Alihi
Wasallam alikuwa akifunga hadi tukadhani kuwa hatofungua kamwe, na alikuwa akiacha
kufunga hadi tukadhani hatofunga tena. Sijamuona Mtume
Salla Llahu 'Alayhi Wa’ala Alihi Wasallam akifunga mwezi mzima kama
isipokuwa Ramadhaan, na sijamuona
akifunga sana –katika siku alizokuwa akifunga- kama alivyokuwa akifunga katika
mwezi wa Shabaan” Imepokelewa na Bukhar,
kitabu cha Sawm, mlango wa Sawm za Shaaban
Ndugu zangu katika
iman, al-Habibu Musttafa (Salla
Llahu 'Alayhi Wa’ala Alihi Wasalla) alikuwa akifunga sana
katika mwezi wa Shabaan kama
ilivyothibiti, na sisi leo tumebakiwa na siku chache sana za mwezi, hivyo hilo
hatukufanikiwa kulipata kwa baadhi yetu.
Ndugu zangu katika
iman, al--Habibu
Musttafa (Salla Llahu 'Alayhi Wa’ala Alihi Wasalla) alikuwa
akifanya yote haya kama ni matayarisho ya kukutana na mgeni mtukufu Ramadhaan, ili iwe wepesi kwake
kutekeleza kwa tawfiq ya Rabbu wa Ramadhaan haya mambo atakapokutana na mgeni mtukufu, na haya
kikweli yanatuhusu sisi (mimi na wewe), kwani yeye hana tatizo katika
kutekeleza a’maali njema, haoni
uzito, na vipi ataona uzito hali amejaaliwa kuwa kipoza macho yake ni katika
Sala, lakini kwa kuwa ameletwa awe kigezo kwa viumbe ndio akawa anafanya
ayafanyayo kwa kuwa tupate kumuiga na sio vyengivyo Allahu a’lam.
Ndugu zangu katika imani, Mgeni wetu ndio yuko milangoni mwetu (anahodisha), na baada
ya siku chache ataingia ndani na kuwa nasi, suala la kujiuuliza ni vipi
tutaisha naye katika kipindi hicho cha mwezi mmoja?
Hili (namna ya kuishi na Ramadhaan) ni somo lenye kujitegea, na
wengi wetu kwa uhaba wa elimu zetu, na shindikizo la tamaduni zetu
zisizokubalika katika Uislamu tunahitaji kuelewa jambo hili, hivyo tukipata
wasaa tutawaomba maustadhi wetu - Allah
awape kila la kheri - watuandalie na kutueleza namna ya kuishi na Mgenu
mtukufu, kwani Mgeni huyu aliyewahi kuwa Mgeni wa al-Habibi Musttafa (Salla Llahu ‘Alayhi Wa’ala Alihi Wasallam) na
Sahaba zake (Radhiya Llahu ‘Anhum),
bila shaka atakuwa anakuja na mbinu na namna ya kuishi nasi, nini anapenda sisi
tukipate kutoka kwake, nini hapendi sisi tufanye, nini afanyiwe ili tufaidike
na ugeni wake, vipi asemezwe ili tupate fadhila zake, na kadhalika
Ndugu Waislamu, mgeni wetu anakuja kwa
lengo la kututayarisha sisi kuweza kufikia lengo lililowekwa na Muumba wetu,
lengo ambalo bila ya kuelewa namna ya kuishi nae itakuwa ni vigumu kulifikia.
Ndugu Waislamu, Ramadhaan inakuja kwa lengo la kutusafisha, kutufunza heshima, utii
na kadhalika, tuwe wavumilivu katika kupata mafundisho yake na tuwe
wastahalimivu katika kukabiliana na mitihani inayotukuta kila siku.
Ndugu Waislamu, Ramadhaan haiwi Ramadhaan kama
hatutokuwa tayari kusameheyana, kukumbushana, kuwaidhiana, kuusiana na
kuamrishana mema na kukatazana maovu katika shughuli zetu zote za kila siku,
kurekebishana kwa namna itayoheshimu kila mmoja utu wake.
Ndugu
yangu katika iman, ningependa kwa tawfiq
yake Mola wa Ramadhaan kuhitimisha
kwa kujaaliya miongoni mwa ya kumkaribisha mgeni Ramadhaan ni
kubainisha/kuainisha au kutaja baadhi ya habarí (hadithi dha’ifu au si sahihah)
zilizo mashuhuri katika ndimi zetu ukiwemo wangu, haya ni kwa kuwa tunatakiwa
kumpokea mgeni kwa kutumia hadithi sio habari, miongoni mwa hizo habari ni:
- “Lau wangeelewa waja yaliyomo katika Ramadhaan wangelitamani umma wangu
iwe Ramadhaan mwaka mzima,
hakika pepo hupambwa kwa ajili ya Ramadhaan
....... “ ni hadithi ndefu.
- “Enyi
watu, umekufikieni/umekufunikeni mwezi mtukufu, mwezi ndani yake umo usiku
ambao ni bora kuliko miezi alfu, amejaalia Allah funga yake ni fardh
na kisimamo cha usiku wake kuwa ni tattawu’
–sunnah sio faradh-, mwenye kujikurubisha ndani ya mwezi huu
kwa (kutenda) jambo lolote la kheri, huwa ni kama aliyetekeleza fardh katika mwezi usiokuwa Ramadhaan, ... na ni mwezi ambao mwanzo wake ni rehmah, katikati yake ni maghfirah, na mwisho wake ni kuachwa
huru na Moto .....” ni hadithi ndefu pia.
- “Fungeni
mtapata afya “
- “Mwenye
kula siku moja katika Ramadhaan bila
ya udhuru wo wote ule wala maradhi, haitalipika siku aliyoiwacha kwa
kufunga dahri kama atafunga“
- “Kila
kitu kila mlango, na mlango wa Ibadah
ni sawm “
- “Usingizi
wa mwenye kufunga ni ibadah “
- “Mambo
matano humfunguza mwenye kufunga: kusema uongo; kusengenya;
kuchochea/kutia fitina; kula yamini ya uongo; na kutazama kwa matamanio “
- “Wanawake
wawili walifunga wakati wa al-Habibi Musttafa (Salla Llahu ‘Alayhi Wa’ala Alihi Wasallam), wakawa kazi yao ni kuwasengenya
watu ....................................... alisema al-Habibi Musttafa(Salla Llahu ‘Alayhi Wa’ala Alihi Wasallam)
hawa wawili wamefunga/wamejizuia na waliyohalalishiwa na Allah, na wamefungua na yale
waliyoharamishiwa na Allah “
Ndugu
zangu katika iman, habari hizi (na
sio hadithi) ni zenye kueleweka kwa wahusika wake, na sio hadithi, hivyo ni
vyema kutozitumia kwani sio hadithi sahihi, na kutumia kama ni hadithi baada ya
kuthibiti kuwa sio ni kumzulia uongo al-Habibu Mustafa (Salla Llahu ‘Alayhi
Wa’ala Alihi Wasallam),
na vipi utakuwa mwenye kujitayarisha
kumpokea Ramadhaan! Huku unamzulia
aliyekuwa yakimuhuzunisha sana yanayo
tutaabisha; aliyekuwa akituhangaikia sana na kwa mimi na wewe -na waumini wote-
kama hatumzulia uongo ni mpole na mwenye huruma sana.
Ndugu zangu katika iman, kilichothibitishwa
na waliotunukiwa na kuruzukiwa macho ya kuona ndani ya hadithi za al-Habibu Mustafa (Salla Llahu ‘Alayhi
Wa’ala Alihi Wasallam) kuwa sio sahihi, ni vyema kwa kila anaepata nafasi
ya kutuwaidhi asitumie habari kama hizi, hata kama maneno/matamshi yake yanaonekana au yanaharufu
ya yote yenye muelekeo na Uislam, lakini sio hadithi za al-Habibu
Mustafa (Salla Llahu ‘Alayhi Wa’ala Alihi Wasallam), na kama hadithi basi sio sahihi, na kuzitumia kama ni hadithi kwa
kusema: amesema al-Habibu Mustafa (Salla Llahu ‘Alayhi
Wa’ala Alihi Wasallam):
hayo, baada ya kuthibiti kuwa sio
sahihi, ni kumzulia uongo al-Habibu Mustafa (Salla Llahu ‘Alayhi
Wa’ala Alihi Wasallam),
na makemeo ya kuzua uongo tunayaelewa vyema, wachilia mbali kumzulia uongo
aliyeletwa kwa lengo la kuigwa nae ni al-Habibu
Mustafa (Salla Llahu ‘Alayhi Wa’ala Alihi Wasallam).
Ndugu Waislamu, tumuombe Rahman atuwafikishe katika kuikaribisha
na kumpokea mgeni wetu Ramadhaan, tumuombe
atuwafikishe katika kuishi na kukaa na Ramadhaan
kwa kuifunga, kutekeleza ayatakayo Muumba, na kuachana na makatazo yake,
pia twamuomba Muumba atupe uwezo wa kufikisha amana kama alivyoifikisha al-Habibu Mustafa (Salla Llahu ‘Alayhi
Wa’ala Alihi Wasallam), atutie mapenzi baina yetu, mapenzi yatayotupelekea
kuwa tayari kusameheyana, kuhurumiana, kuvumiliana, kuheshimiana na kukosoana
na kurekebishana kwa njia na namna alivyokuwa akiwarekebisha al-Habibu Mustafa (Salla Llahu ‘Alayhi
Wa’ala Alihi Wasallam) Sahaba zake (Radhuya
Llahu ‘Anhum).
Wassalamu'alaykum
Warahmatu Llahi Wabarakatuh
Imekusanywa na
Ndugu yenu katika imani
Abu Faatimah
No comments:
Post a Comment