Habari za Punde

Waliohamishwa Kiwira walipwa chao

Na Thompson Mpanji, MBEYA
SERIKALI imeanza kuwalipa mafao ya wafanyakazi 398, walioachishwa kazi katika mgodi wa makaa ya mawe Kiwira, wilayani Kyela mkoani Mbeya na kuwapatia muda wa miezi mitatu kuishi katika nyumba zinazomilikiwa na ngodi huo.
 
Akizungumza na wafanyakazi hao katika ukumbi wa mgodi huo, Mkurungenzi wa Fedha na Utawala STAMICO, Peter Gembe, alisema kuwa serikali kupitia wizara ya Nishati na Madini imetoa shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya malipo ya wafanyakazi na watalazimika kuondoka ifikapo Septemba 30 mwaka huu.
 
Alisema kazi ya kuwalipa mafao wafanyakazi hao itadumu kwa muda wa wiki moja ikiwa pamoja na kuishirikisha mifuko ya fedha kwa wafanyakazi kama NSSF na PPF kupiga kambi katika eneo hilo ili kuhakikisha kuwa wafanyakazi hao walioachishwa kazi wanapata malipo ya michango yao waliyokuwa wanachangia.
 
Gembe alisema kuwa baada ya kumalizika kwa zoezi hilo STAMICO imejipanga kuendesha mgodi huo pamoja na kujiwekea lengo la kutaka kuendesha  kisasa zaidi kwa kuleta vifaa vipya na kubadilisha mfumo wa uchimbaji wa makaa.

Alifahamisha kuwa mgodi huo utakapoanza kazi utakuwa na uwezo wa kuzalisha  zaidi ya tani  milioni moja kwa mwaka pamoja na kuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 200 za umeme ambazo zitaingizwa moja kwa moja katika gridi ya taifa ili kuondokana na tatizo la umeme nchini.
 
Alisema kuwa mgodi huo mara utakapoanza kazi utatoa ajira zaidi ya 1,000 kwa wafanyakazi wapya ikiwa ni tofauti ya wafanyakazi waliokuwepo awali 500 na kuwaasa wafanyakazi walioachishwa kazi huku wakiwa bado wanazo sifa za kufanya kazi katika mgodi huo wavute subira ya kuomba upya kazi.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya Kyela Magreth Malenga, aliwataka wafanyakazi hao kukubali kile ambacho serikali imekubali kuwalipa na kuwataka wale watakaolipwa kuhakikisha wanaondoka haraka kwenye nyumba hizo za mgodi ili kupisha serikali kupanga mipango endelevu kuhusiana na mgodi huo
 
Aidha amewaasa wafanyakazi hao kutulia na ndoa zao mara baada ya kupata mafao yao kwa maana ya kutafakari kwanza kabla kukurupuka kwani itawasaidia kuzitumia pesa hizo ipasavyo na kupambana na mazingira mapya wanayokwenda kuishi.
 
Wakati zoezi hilo likiendelea baadhi ya wafanyakazi walioachishwa kazi katika mgodi huo na kupokea hundi zao za fedha walionyesha kutoridhishwa na mafao waliyopata ambapo wamedai kuwa fedha waliyoipata ni kidogo kiasi kwamba hazitawawezesha kuishi maisha mapya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.