Habari za Punde

Dk. Salmin: SUZA ifundishe fani za utabibu. Asema itapunguza gharama za tiba., Adokeza lengo la kuanzishwa chuo hicho.

Na Haroub Hussein
RAIS Mstaafu wa awamu ya tano wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma amesema umefika wakati kwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), kufundisha shahada ya Udaktari wa tiba.

Dk. Salmin alieleza hayo huko nyumbani kwake Migombani mjini Zanzibar, alipokuwa akizungumza na uongozi wa Chuo hicho uliofika kumkabidhi shahada yake ya Uzamifu ya Heshima iliyomtunuku.

Alisema kuanzishwa kwa mafunzo ya tiba, kutasaidia kuwaondoshea matatizo mbali mbali wananchi wa Zanzibar, ikiwa ni pamoja na kuwapunguzia gharama za kufuata matibabu nje ya nchi.

Dk. Salmin alisema ni vyema SUZA, katika mipango yake ikafikiria suala la kuanzisha shahada hiyo kwa lengo la kuisaidia jamii nzima ya Afrika ambayo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa wataalamu wa tiba, huku wananchi wengi katika eneo hilo wakikabiliwa na matatizo mbali mbali ya kiafya.

Alisema wananchi wengi wamekuwa wakisumbuka kutafuta tiba za maradhi yanayowakabili nje ya nchi jambo ambalo kutokana na umasikini wao hawalimudu kutokana na ukubwa wa gharama zake.

"Ni vyema mkaanzisha masomo ya Udaktari wa tiba kwani Afrika bado hatuna tiba ya kutosha watu wengi, maradhi mengi lakini matibabu bado tatizo hivyo ni vyema tukajikita katika suala hili kwa lengo la kuisaidia jamii yetu",  alishauri Dk.Salmin.

Aidha alisema katika kufikia azma hiyo Chuo kitafute eneo kubwa litakaloweza kujenga Chuo cha tiba kitachokua mfano kwa Afrika nzima ambacho kitaweza kuitangaza Zanzibar kutokana na ubora wake.

Akizungumzia historia ya kuanzishwa kwa kwa SUZA, Dk.Salmin alisema wakati akiwa Rais alitoa wazo la kuanzishwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, baada ya kuona madhila wanayoyapata wanafunzi wa Zanzibar katika suala la elimu ya juu.

Alisema madhila hayo yalimkumbusha historia ya maisha yake wakati akitafuta elimu miaka ya 1961 alipokwenda Dar es Salaam kwa jahazi na kukwama siku tatu baharini huku Dar es salaam akiwa hana jamaa wala pesa.

"Madhila waliyokuwa wakiyapata wanafunzi wa Zanzibar yalinikumbusha maisha yangu halisi wakati nikitafuta elimu ambapo siku ya Jumanne tarehe 23 mwaka 1961 alipopanda jahazi kuelekea Dar es salaam ambapo walipofika katika mkondo wa kibaazi tulikubwa na dhoruba jambo lililotufanya tukwame siku tatu baharini”,alisema Dk. Salmin.

Alifahamisha kuwa baada ya kufika Dar es salaam, alijitambulisha kwa wazee wa Chama cha TANU, alipoamrishwa waziri wa Mambo ya Nje kumtafutia skuli na sehemu ya kuishi ndipo alipopelekwa skuli ya Aga ghan na gharama zote zililipwa na serikali ya wakati huo.

Dk. Salmin alisema aliamua kuunda tume ya watu watano kukusanya mawazo kwa lengo la kuanzisha Chuo hicho, tume ambayo wajumbe wake walikuwa ni pamoja na Marehemu Prof.Haroub Othman, Prof.Saleh Idrisaa na wenzao watatu ambapo waliendelea na mchakato huo hadi muda wa uongozi wake unamalizika na ulipoingia uongozi wa Amani Karume Chuo hicho kikaanza rasmi.

"Naupongeza sana Uongozi wa SUZA kwa kunitunuku shahada hii ya udaktari wa heshima kwa mchango wangu pia nakupongezeni kwa kuanzisha shahada ya udaktari wa lugha ya Kiswahili hilo ni jambo la kujivunia kwa Zanzibar", alisema Dk.Salmin.

Nae Makamu Mkuu wa Chuo hicho,Prof.Idris Ahmada Rai alisema miaka 10 ya Chuo wamejipanga kupanua wigo kwa kuwa na skuli nne kutoka moja ya awali wakati chuo kinaanzishwa, akizitaja skuli hizo kuwa ni skuli ya Kiswahili na lugha za Kigeni, skuli ya elimu, skuli ya sayansi ya maumbile na jamii pamoja na skuli ya elimu ya kitaalamu na endelevu.

Prof. Rai alisema kuanzia mwaka mpya wa masomo unaoanza mwezi wa Oktoba mwaka huu Chuo kitaanzisha masomo ya Udaktari wa lugha ya Kiswahili ambapo hatua huyo imefikiwa baada ya Maprofesa wengi wa Kizanzibari kuamua kurudi nyumbani kuja kufundisha Wazanzibari wenzao.

Akitoa shukrani mjumbe wa Baraza la Chuo hicho, Mohammed Said Dimwa alisema SUZA inathamini mchango wa Dk.Salmin na haitosita kuendelea kumtumia kwa ushauri maelekezo pale itapoona inafaa kwa maendeleo ya chuo.

Chuo cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimeanzishwa mwaka 2002 kwa sheria namba nane ya mwaka 1999 ya Baraza la Wawakilishi kilianza na wanafunzi 55 ambapo hivi sasa kina wanafunzi wapatao 2000.

 

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.