Habari za Punde

Dk Shein atuma salamu za rambirambi kifo cha Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi

Na Rajab Mkasaba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, amemtumia salamu za rambi rambi Rais wa Ethiopia Mhe. Woiddegiorgis Girma, kufuatia kifo cha Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mhe. Meles Zenawi.

Katika salamu hizo Dk. Shein alisema kuwa wananchi wa Zanzibar wamepokea kwa  mshtuko, masikitiko na huzuni  kubwa  taarifa ya kifo cha Waziri Mkuu huyo kilichotokea  juzi usiku.

Salamu hizo zilieleza kuwa Dk. Shein pamoja na wananchi wa Zanzibar wanaungana na ndugu zao wa Ethiopia katika msiba huo mkubwa uliolikumba taifa hilo.

Dk. Shein amesema kuwa “Kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar, Serikali na mimi mwenyewe, natuma salamu za rambirambi kwako na kwa ndugu zetu wa Ethiopia”.
 
Salamu hizo za rambi rambi zilieleza kuwa Zenawi atakumbukwa kwa msimamo wake thabiti wa kutetea maslahi ya Afrika na ustawi wa watu wake  pamoja na kupigania maendeleo ya kiuchumi si kwa Ethiopia tu bali kwa bara zima la Afrika.

Sambamba na hayo, salamu hizo ziliendelea  kueleza kuwa Waziri Mkuu huyo alikuwa mashuhuri katika kupigania umoja na mshikamo wa  Afrika. “Afrika imepoteza mtu madhubuti, watu wa Zanzibar wanaungana na watu wengine duniani katika kutoa salamu zao kwa kiongozi huyu mashuhuri kufuatia kifo chake’zilieleza salamu hizo.

Salamu hizo, zilimuomba MwenyeziMungu awape moyo wa subira na uvumilivu wanafamilia pamoja na wananchi wote wa Ethiopia na kumuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya kiongozi huyo katika amani.

Waziri Mkuu Zenawi amefariki dunia akiwa na  umri wa miaka 57 ambaye amekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia tokea mwaka 1995 na kabla ya hapo alikuwa Rais wa nchi hiyo kati ya mwaka 1991 na 1995.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.