Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Leodgar Tenga, amewaomba radhi waandishi wa habari kutokana na adha waliyoipata wakati wa fainali za Kombe la Kagame kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Katika tukio hilo, waandishi walizuiwa kuingia kwenye uzio wa uwanja huo kufanya mahojiano mara baada ya kumalizika kwa mechi ya fainali kati ya Yanga na Azam FC, ambapo baadhi yao walinyanyaswa kwa namna moja au nyengine.
Akizungumza na wahariri wa michezo kwenye makao makuu ya TFF, Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Michezo Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, (CECAFA), alisema yeye ni muumini wa haki, hivyo amesikitishwa na hali iliyojitokeza, hivyo anaomba radhi na asingependa hali hiyo iendelee tena.
“Mimi ni muumini wa haki, nawaomba radhi na kuwapa pole wale waliopata misukosuko siku ile, sioni kwa nini hili linajitokeza. Nikiwa Rais wa TFF na Mwenyekiti wa CECAFA nawaomba radhi, halileti ‘image’ nzuri, hata kama kulikuwa na tatizo, ni vyema kuelekezana lakini si kwa hali hii,” alisema Tenga.
Tenga aliwataka viongozi wa TFF, Katibu Mkuu na Ofisa Habari, kukutana na viongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), ili kujadili hali hiyo na kuweka mambo sawa ili isije ikatokea tena huku akisisitiza, njia ya majadiliano ndio muafaka wakati wote.
Awali kutokana na mtafaruku huo, TASWA ilitangaza mgogoro na kufikia uamuzi wa kususia masuala yote yanayolihusu baraza hilo.
Mwenyekiti wa Taswa Juma Pinto, amesema chama chake kimepokea na kukubali radhi iliyoombwa na TFF, akisema mtu kukosea na kukubali makosa kisha akaomba radhi huo ni muungwana.
Hata hivyo, amesema chama chake kitafanya kikao na sekretarieti ya TFF kwa ajili ya kujadili namna bora ya kushirikiana ili kadhia kama hiyo isitokee tena.
No comments:
Post a Comment