Na Haji Nassor, Pemba
TIMU ya Chipukizi inayoshiriki ligi kuu ya soka Zanzibar, imeimarisha kikosi chake kwa kusajili nyota sita wapya kwa ajili ya kuitumikia katika msimu ujao unaotarajiwa kuanza Septemba 8, mwaka huu.
Kocha wa klabu hiyo Issa Kassim, amewataja wanandinga hao na timu wanazotokea zikiwa kwenye mabano, kuwa ni Vuai Abdallah (Africana daraja la pili Chake Chake), mlinda mlango Foum Yussuf (Duma), Ali Hemed (Vikunguni), Seif Ali (Machomane United) na Abdullatif Ali iliyemnyakua kutoka timu ya Makombeni.
Hata hivyo, timu hiyo imeamua kuwatema wachezaji wake wawili, huku mlinda mlango wake nambari mbili Saleh Abdallah Kassim, akihama na kujiunga na watoza ushuru wa Zanzibar Forodha yenye maskani yake kisiwani Unguja.
Wachezaji walioenguliwa kikosini humo, ni Haji Rashid anayechezea nafasi ya ulinzi, na Ali Abbass ambaye ni mshambuliaji.
"Nina imani usajili huu tulioufanya, utasaidia kuiimarisha zaidi timu yetu, kwa sababu msimu uliopita baadhi ya maeneo yalikuwa dhaifu, lakini kwa sasa wamepatikana wachezaji wanaofiti na kikosi kiko tayari kwa mapambano", alijigamba kocha huyo.
Aidha alifafanua kuwa, msimu huu timu yake haikusajili wachezaji kutoka nje ya Zanzibar, kwa vile walionao sasa wanaendelea vizuri na mchango wao kwa msimu uliopita ulionekana, akisema bado wachezaji waliowasajili kutoka Bara kina Sadik, Abdullatif Ali, na Kimathi, wanaendelea kukipiga na timu hiyo.
Alihitimisha kwa kueleza matumaini yake kuwa kupatikana kwa mdhamini wa ligi kuu msimu ujao, kutasaidia kuleta msisimko na kukuza ushindani, huku akikitaka Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kiwe makini kwa kutowakumbatia waamuzi wanaoendekeza rushwa na kuivuruga ligi hiyo.
No comments:
Post a Comment