NAIBU Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu Issa Haji Ussi, kesho anatarajiwa kufunga mkutano wa Shirikisho la Mashindano ya Magari barani Afrika (AAT), utakaofanyika katika hoteli ya Blue Bay iliyoko Kiwengwa Wilaya ya Kaskazini B.
Mkutano huo wa mwaka umeandaliwa kwa ushirikiano na
shirikisho kama hilo
la dunia (FIA), pamoja na Baraza la Afrika la michezo ya vyombo vya moto na
utalii (ACTA).
Mratibu wa mkutano huo hapa Zanzibar Mussa Tharia, amezitaja
nchi hizo kuwa ni Kenya, Uganda, Tanzania, Botswana, Afrika Kusini, Nigeria,
Msumbiji, Zimbabwe, Malawi na Zambia.
Tharia amesema, mkutano huo pia utahudhuriwa na Makamu wa
Rais wa Baraza la Michezo ya Vyombo vya Moto wa dunia, ambaye pia ni Rais wa
klabu ya michezo hiyo ya Falme za Kiarabu (UAE), Dk. Mohammed Ben Sulayem,
atakaeuongoza ujumbe wa watu sita.
Mratibu huyo amesema, mkutano huo hauna lengo la kuyarejesha
mashindano ya magari hapa Zanzibar ,
lakini umevutiwa na mandhari ya kisiwa hichi chenye vivutio vya kitalii ambapo alisema
ujio wa wajumbe wake, unakadiriwa kuingiza takriban dola 40,000 (62,800,000
Tshs).
Hata hivyo, alisema kuna michezo tafauti inayohusisha magari
ambapo kunakuwa na viwanja maalumu vilivyojengewa uzio, na wachezaji huzunguka
na kuonesha umahiri wa kuendesha huku watazamaji wakiwa majukwaani katika hali
ya usalama.
“Kama itaona iko haja, Zanzibar
inaweza kuanzisha michezo kama hiyo ambayo huchezwa katika mazingira salama”,
alieleza Tharia ambaye ni Katibu wa klabu ya mashindano ya magari hapa Zanzibar , ambayo alisema
bado haijafa.
Kimsingi, alisema mktano huo utajadili njia bora za
uendeshaji salama wa magari unaolenga kupunguza ajali na majanga yatokanayo na
vyombo vya moto iwe michezoni au katika safari za kawaida.
Miongoni mwa wajumbe watakaohudhuria mkutano huo wa mwaka,
ni Rais wa FIA kanda nambari moja, Werner Kraus, Mkurugenzi Mwendeshaji na Rais
wa Afrika David Njoroge, na Katibu Nizar Jivani kutoka Tanzania, ambaye ni Rais
wa AA Tanzania, pamoja na Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa.
Zanzibar iliwahi kuandaa mashindano ya magari Tanzania kwa
mara ya kwanza mwaka 2005 ambayo yalimalizika salama, na baadae mwaka 2006 na
2007, ambapo kwa bahati mbaya kulitokezea ajali zilizosababisha vifo vya madereva Nasir Khan (2006) na Khalid Bakhresa
(2007).
Kufuatia matukio hayo, Serikali ya Zanzibar ilitangaza kuyasitisha hadi muda
usiojulikana.
No comments:
Post a Comment