Habari za Punde

Zanzibar Heroes yawasili Zanzibar

Na Faki Mjaka Maelezo Zanzibar- 10/12/2012
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema imefurahishwa sana na kiwango cha mchezo kilichooneshwa na Timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) katika Mashindano ya Challenge licha ya kuambulia mshindi wa tatu wa mashindano hayo.
Aidha katika kuipongeza Timu hiyo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein amepanga kukutana na Vijana hao ikiwa ni pamoja na kubadilishana mawazo ya kuimarisha kikosi cha Timu hiyo.
Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Bihindi Hamad Khamis ameyasema hayo ukumbi wa Hoteli ya Bwawani wakati alipokuwa akizungumza na Timu hiyo mara baada ya kuwasili Zanzibar kutoka Uganda.
"Naleta salamu Rasmi za Serikali kwa juhudi kubwa mliyoifanya kule Uganda na Rais kasema atapanga siku ya kukutana na nyinyi ili mbadilishane naye mawazo ya kuboresha timu zaidi" alisema Bihidi.
Amesema juhudi ambazo zilioneshwa na Vijana wa Zanzibar Heroes zinafaa kuthaminiwa kutokana na kucheza na timu ziliozojaa uzoefu na wachezaji maarufu lakini vijana hao walipigana kiume na kuambulia nafasi ya tatu.
Bihindi amewataka Wachezaji wa Zanzibar Heroes kutunza afya na kuimarisha mazoezi yao ili michuano ya mwakani waweze kuwaletea Wazanzibar kikombe cha Ushindi wa Mashindano hayo.
Ameongeza kuwa kiwango cha mchezo walichoonesha vijana hao kiliwasisimua Wazanzibari wengi na kuwasababisha kutenga muda wao kwa ajili ya kuangalia timu yao kila ilipokuwa ikicheza.
Aidha aliwataka Wachezaji hao kuitumia fursa ya kuonana na Rais kuelezea mipango wanayodhani itakuwa bora katika kuimarisha Timu hiyo kwa faida yao na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Meneja wa Timu ya Zanibar Heroes Salim Msabah ameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kushirikiana bega kwa bega na Chama cha Soka Zanzibar ZFA katika kuhakikisha timu inapatiwa maandalizi ya mapema ndani na nje ya Nchi ili kuimarisha kikosi cha timu hiyo.
Amesema anaamini Zanzibar kuna vipaji vya kutosha katika fani ya Soka na hivyo kinachohitajika ni namna bora ya kuviendeleza vipaji hiyo ikiwa ni pamoja na maandalizi ya mapema.
Nahodha wa Timu hiyo Nadir Haroub amesema lengo lao lilikuwa kutwaa Ubingwa wa Michuano hiyo lakini nafasi waliyoipata ya Mshindi wa tatu imewafariji kutokana na kuifunga timu pinzani kwao.
Amedai kuwa ushindi huo pia utawajengea heshima wale wachezaji wa Zanzibar wanaocheza Soka katika ligi ya Bara kutokana na kuifunga Kilimanjaro Stars ambayo wanacheza wake wanacheza wote katika ligi hiyo.
Timu ya Zanzibar Heroes iliibuka Mshindi wa Tatu wa Mashindano ya Challenge yaliyofanyika nchini Uganda baada ya kuichapa Kilimanjaro Stars kwa mikwaju ya Penalti 6-5 na kufanikiwa kupata zawadi ya kitita cha Dola za Marekani 10,000.

1 comment:

  1. Asante kwa kutupasha habari hizi, hivi ndivyo tunavyotaka babari zilizoambatana na picha, na sio mtuekee mapicha matupu kama tunaangalia albamu za harusi.

    Hongereni Zanzibar Herroes.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.