Habari za Punde

Bibi kizee ateketea kwa moto akiwa usingizini



Joseph Ngilisho,Arusha
BIBI kizee mwenye umri wa miaka 85,Elishusa Zakaria mkazi wa kijiji
cha Mfuloni,kata ya Ndohombo wilaya ya Arumeru,mkoani Arusha,amefariki duni kwa moto nyumbani kwake, akiwa usingizini.

Tukio hilo limefahamika mara baada ya kugundulika mwili wa marehemu, jana majira ya saa 5:30 asubuhi baada ya mjukuu wake aliyefahamika kwa jina la Janeth Peterson(16)alipoenda nyumbani kwa
bibi yake kumtembelea.

Akizungumzia tukio hilo,Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha,Liberatus
Sabas alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa chanzo cha tukio hilo ni kibatali kilichokuwa kikiwaka na baadae kuripuka na moto kusambaa kwenye godoro alililokuwa amelalia.


“Katika nyumba hiyo yenye vyumba vitatu marehemu alikuwa amelala
kwenye chumba kimojawapo na inaonyesha hapa kuwa na mtu mwingine anayeishi naye,”alisema Kamanda huyo.


Aidha mbali na kifo cha marehemu, baadhi ya vitu vilivyoko ndani ya
chumba hicho vikiwemo vyakula,vyombo, kitanda na godoro
viliungua ,huku thamani yake bado haijafahamika ambapo polisi
wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Mwili wa marehemu umezikwa baada ya kufanyiwa uchunguzi na daktari na
kuukabidhi kwa ndugu wa merehemu.

Wakati huo huo,mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Laray mwenye umri wa miaka 25 mfanyakazi wa kampuni ya ujenzi iitwayo Shereji Construction  amefariki dunia  baada ya gari alilokuwa akisafiria
kuacha njia na kupinduka.

Kamanda wa polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas alisema tukio hilo
lilitokea Febuari 20 mwaka huu majira ya saa 1:15 jioni katika eneo la chuo kikuu cha Nelson Mandela wilayani Arumeru.

Alisema siku ya tukio  gari aina ya Toyota Hilux lenye namba za
usajili T 732 AEF lililokuwa linaendeshwa na Rajkumar Sharma (24) mkazi wa Kijenge lilipinduka na kusababisha kifo cha mtu huyo.

Sabas alisema,ajali hiyo ilitokea wakati gari hilo likiwa linatokea maeneo ya Usa river kuelekea mjini na ilipofika karibu na lango kuu la chuo hicho lilianguka na kusababisha kifo  cha abiria
huyo baada ya kuegemewa na gari hilo.

Aidha chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana na jeshi la polisi
mkoani hapa linaendelea  na uchunguzi zaidi ili kujua chanzo halisi na dereva huyo anaendelea kuhojiwa na atafikishwa mahakani pindi upelelezi utakapokamilika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.