WAZIRI wa Makaazi, Maji, Nishati na Adhi, Ramadhan Abdulla Shaaban,
ameitaka Bodi ya Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), kusimamia ipasavyo sheria ya
uungaji maji, ili kudhibiti wimbi la uungaji wa maji kiholela, unaosababisha
upungufu mkubwa wa huduma hiyo.
Waziri huyo alitoa changamoto hiyo jana
katika ukumbi wa Mamlaka ya Maji Gulioni, katika uzinduzi wa bodi ya
tatu ya Wakurugenzi ya Mamlaka hiyo.
Alisema Mamlaka hiyo inakabiliwa na jukumu kubwa la kutatua tatizo sugu la
uungaji maji kiholela, unaofanywa na baadhi ya mafundi wa mamlaka kwa
kushirikiana na wananchi, kinyume na taratibu na miongozo ya utumishi.
Alisema hatua hiyo isiozingatia sheria wala
utaalamu inapelekea uharibifu wa mfumo wa miundombinu na kuwa chimbuko
la upungufu wa maji, hususan katika maeneo ya mjini.
“Mafundi wa ZAWA kamwe wasihusike na uungaji wa maji katika miradi ilio nje
ya mamlaka hii,” alionya.
Aidha alisema pia kuna tatizo kubwa la uchimbaji holela wa visima, ambao
huwanufaisha wananchi wachache wenye uwezo na kupelekea wananchi wengi kukosa
huduma hiyo muhimu.
Waziri huyo aliwataka wajumbe wa Bodi hiyo kusimamia utoaji wa elimu kwa
wananchi ili waweze kufahamu matumizi bora ya maji, pamoja na uhifadhi wa
mazingira na vianzio vyake.
Katika hatua nyingine Waziri Shaaban, aliwataka wajumbe wa Bodi hiyo pamoja
na wataalamu wa ZAWA kufanya kazi kwa mashirkiano ilii kuleta ufanisi na
upatikanaji wa uhakika wa huduma hiyo.
Nae, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mustafa Aboud Jumbe alisema hivi
sasa dunia inakabiliwa na changamoto kubwa ya mabadiliko ya hali ya hewa, hatua
inayopelekea upungufu mkubwa wa maji, hivyo kuitaka Mamlaka ya Maji
kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kutunza vianzio vya maji.
Mapema Mwenyekiti wa Bodi hiyo,
Mtumwa Khatibu Ameir, alisema suala la upatikanaji wa maji safi na salama ni tete kwa kuzingatia kuwa linakabiliwa na
changamoto nyingi, ikiwemo uchakavu wa miundo mbinu.
Aliitaka mamlaka hiyo kuwashajiisha wananchi kuchangia huduma hiyo kwa
mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.
No comments:
Post a Comment