Na Himid Choko,BLW
SHIRIKA la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)
limekabidhi msaada wa gari tatu kwa ajili ya matumizi ya Kamati za Kudumu za
Baraza la Wawakilishi.
Gari hizo zilizogharimu kiasi ya shilingi milioni 152 ni
miongoni mwa misaada ya shirika hilo chini ya mradi wa kusaidia mabunge.
Akikabidhi msaada huo kwa Spika wa Baraza la Wawakilishi,
Pandu Ameir Kificho, Mkuu wa Ofisi ya UNDP Zanzibar, Anna Segan alisema shirika lake limetoa msaada huo ili
kuzijengea uwezo zaidi kamati hizo.
Alisema kamati za kudumu za mabunge ni vyombo
vinavyopaswa kujitegemea ili kutekeleza kazi zake kwa ufanisi zaidi.
Alisema kazi ya
kusimamia na kuchunguza serikali
na taasisi zake ni muhimu na ngumu hivyo
Kamati za Kudumu za Mabunge
pamoja na mabunge yenyewe yanapaswa kuwa na vitendea kazi vya
kutosha ili ziweze kuheshimika kwa wanaowachunguza na kuwasimamia.
Aidha alisema kwamba serikali nyingi ulimwenguni
zimefanikiwa kiutendaji na uwajibikaji kutokana na usimamizi mzuri na madhubuti
unaotokana na kamati za mabunge.
Akipokea msaada huo Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu
Ameir Kificho alisema Baraza la
Wawakilishi na serikali inaridhishwa na juhudi za UNDP kwa misaada yake mbali mbali nchini.
Alisema shirika hilo limekuwa mstari wa mbele katika
kusaidia maendeleo ya wananchi na kuendelea kutoa wito kwa mashirika mengine
kuiga mfano huo.
Alisema kupatikana
kwa gari hizo kutasaidia
kurahisisha usafiri kwa kamati za
kudumu na hivyo kuwawezesha kuwa huru zaidi katika kutekeleza majukumu yao
ambapo awali mara nyingi walikuwa wakitegemea usafiri kutoka taasisi wanazozifanyia kazi.
Nae Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad
ameahidi kwamba ofisi yake itazitunza gari hizo na zitatumika kama
ilivyokusudiwa.
No comments:
Post a Comment