Habari za Punde

Mufti Mkuu ahimiza upendo, mshikamano


Na Laylat Khalfan

VIONGOZI wa dini Zanzibar, wameelezea wasiwasi juu ya vitendo vya mauaji ya viongozi wa dini vinavyotokea siku hadi siku nchini.
Hayo yalielezwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi,alipozungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake  Mazizini juu ya tukio la mauaji ya Padri Evarist Mushi.
Alisema vitendo hivyo ni matukio ya watu wasioitakia mema Zanzibar  na havina uhusiano wa kidini kwa sababu dini zote zimekataza binadamu kuchukua hatua ya kumuua mwenzake.

Sheikh Kabi alisema tukio la kuuliwa kwa Padri Mushi limewahuzunisha wanachi na waumini wa dini ya kiislamu kwani wote wanaishi kwa amani na upendo.
Aidha aliwataka wananchi kuachana na vitendo vya uhalifu vinavyosababisha uvunjifu wa amani na kuwaomba viongozi wa dini kuwaelimisha waumini wao kuwa watu wema wanaopendana.
Alifahamisha kuwa ni vyema kwa vyombo vya ulinzi kufanyakazi kwa uhakika ili kudhibiti mtandao unaohatarisha amani iliyodumu kwa muda mrefu Zanzibar.
Nae Mwalimu wa Idara ya Vijana wa Waumini ya dini ya Kikiristo Zanzibar, David Vikta Suna, alisisitiza kuwepo kwa ushirikiano kati ya serikali na wananchi ili kuona vitendo hivyo vinadhibitiwa na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.