Said
Ameir, Ikulu
RAIS
wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza dhamira ya
dhati ya serikali kuendeleza na kuimarisha sekta ya utalii kwa kushirikiana na
washirika wa sekta hiyo ikiwemo sekta binafsi.
Dk.
Shein alitoa kauli hiyo jana Ikulu wakati wa mazungumzo na Bodi ya Wakurugenzi
wa Jumuiya ya Wawekezaji katika sekta ya utalii Zanzibar (ZATI) na Jumuiya ya
Makampuni ya Watembeza Watalii Zanzibar (ZATO).
“Dira
yetu ya maendeleo ya mwaka 2020 inatuelekeza kuwa utalii ndio sekta mama na
halikadhalika mpango wetu wa kupunguza umasikini Zanzibar (MKUZA II) umetilia mkazo sio tu
nafasi ya sekta ya utalii katika kupambana na umasikini bali pia maendeleo yetu
kwa ujumla,” alisema Dk. Shein.
Dk.
Shein alizipongeza bodi na viongozi wa ZATI na ZATO kwa ushirikiano wao na serikali
na taasisi zake kama vile Mamlaka ya Ukuzaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya
Mapato Zanzibar (ZRB) ushirikiano ambao aliueleza kuwa umesaidia kukuza sekta
hiyo Zanzibar.
Alibainisha
kuwa madhumuni ya kuleta dhana ya utalii kwa wote ni kuhakikisha kuwa kila
mmoja anashiriki kwa nafasi yake na mahala alipo kwa namna moja au nyingine
katika kukuza na kuimarisha utalii Zanzibar.
“Tunataka
kila mtu ashiriki kukuza na kuimarisha utalii kwa sababu ndio sekta yetu kuu ya
uchumi na inatufaidisha sote kwa namna moja au nyingine,” alifafanua Dk. Shein.
Katika
mazungumzo hayo ambayo yalihudhuriwa pia na Mshauri wa Rais masuala ya Utalii,Issa
Ahmed, ujumbe wa ZATO na ZATI walibadilishana mawazo na Rais kuhusu masuala ya
huduma katika sekta ya utalii, usalama wa watalii, kuitangaza Zanzibar nje kuvutia
uwekezaji na kuongeza idadi ya watalii pamoja na haja ya kuimarisha mafunzo kwa
wananchi wa Zanzibar ili kuongeza ajira kwa Wazanzibari katika sekta hiyo.
Kwa
hiyo alitoa wito kwa wadau wote katika sekta ya utalii na zile ambazo
zinahusiana na sekta hiyo pamoja na wananchi kushirikiana kwa hali na mali
kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo muhimu kwa
maendeleo ya Zanzibar.
Aliwahakikishia
washirika wa sekta ya utalii kuwa milango ya serikali yake iko wazi kwa
majadiliano ya mara kwa mara kuhusu namna bora ya kuimarisha sekta ya utalii
nchini.
Katika
mazungumzo hayo ujumbe wa ZATI uliongozwa na Mwenyekiti wake, Abdulswamad Said
Ahmed na ule wa ZATO uliongozwa na Mwenyekiti wake, Khalifa Mohamed Makame.
No comments:
Post a Comment