Mbunge wa Makunduchi ambaye pia ni Waziri anayeshughulikia masuala ya Muungano, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanajumuiya wa maendeleo ya watu wa Mzuri na wageni wao kutoka Sweden.
Picha hii imepigwa mbele ya jengo la walimu baada ya kulikagua. Pamoja na mambo mengine Mhe. Samia amefungua mradi wa maji Mzuri Kaja na kituo cha mawasiliano ya habari (ICT center) kilichopo katika club ya mpira ya Jamhuri Makunduchi.
Kituo hichi kimefunguliwa na wanajumuiya ya maendeleo ya Makunduchi (Makunduchi Development Society) baada ya kutafsiri muono (vision) ya Mhe. Samia ambaye anataka kuligeuza jimbo la Makunduchi kuwa kimbilio kwa elimu ya kompyuta.
Kwa lugha nyengine Mhe. Waziri anataka jimbo lake kuwa "mini-silicon valley" kwa Zanzibar na Tanzania kwa jumla. Kituo cha kompyuta cha Makunduchi kinategemewa kuwa na kompyuta 100 ambazo zitaunganishwa na mtandao.
Kituo hicho pia mbali na kutoa mafunzo ya kompyuta kitafundisha pia hisabati na lugha ya kiingereza ili kurahisisha mafunzo ya kompyuta.
Mheshimiwa Samia ameahidi kukipatia kituo hicho vipoza hewa. Ziara ya Mheshimiwa Samia alikuwa ya mafanikio makubwa na amejenga moyo ya kujitolea zaidi kwa watu wa Makunduchi ambao wamempongeza kwa jitihada zake za kuleta maendeleo endelevu jimboni hapo
No comments:
Post a Comment