Habari za Punde

Majambazi yapora 2.5m/- Pemba



Na Masanja Mabula,Pemba
WATU wanaosadikiwa kuwa majambazi usiku wa kuamkia Jumapili wamevamia  nyumbani kwa Juma Haji Kombo (Malengo) mkaazi wa shehia ya Mzambarautakao wilaya ya Wete na kufanikiwa kupora shilingi milioni 2.5 pamoja vitu vya dhabhabu na simu nne  za mkononi.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kaimu Kamanda wa polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Juma Sadi alisema katika tukio hilo majambazi hao walikuwa ni wanane na mara baada ya kutekeleza tukio hilo walikimbia katika mabonde ya  msitu wa Matuuni Mtambwe.
Alisema tukio hilo limetokea usiku wa saa 2 :10 ambapo walipoingia ndani walimlazimisha kutoa pesa huku wakitishia kumuua ambapo aliwakabidhi  fedha kwa hofu ya usalama wa maisha yake.

Kamanda Sadi amefahamisha jeshi la polisi mkoa huo lilipata taarifa ya kuwepo na tendo la uhalifu katika shehia ya Mzambarautakao, hata hivyo hawakuweza kufanikiwa kuwakamata majambazi hao.


Naye Naibu sheha wa Shehia hiyo, Mwanajuma Mohammed akizungumza na mwandishi wa habari hizi ameitaka jamii  kuimarisha mpango wa ulinzi wa polisi jamii ili kuweza kusaidia kudhibiti matendo kama hayo.

Alisema kwamba kuwepo kwa ulinzi shirikishi ndio  njia pekee ya kuweza kuwabana wahalifu kwani itakuwa ni rahisi kufichua maficho ya wanaojighusisha na vitendo hivyo .

Tukio hilo ni la pili kutokea katika Wilaya ya Wete katika kipindi cha mwaka huu, ambapo tukio kama hilo lilitokea wiki  mbili zilizopita kwa Afisa Mdhamini Wizara ya Miundo Mbinu na Mawasiliano Pemba kuvamiwa na majambazi akiwa nyumbani kwake Kifumbikai.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.