Habari za Punde

ZRB yakusanya 67b/-



Na Husna Mohammed
 
BODI ya Mapato Zanzibar (ZRB), imekusanya shilingi bilioni  67.642 sawa na asilimia 82.65 kuanzia mwezi Julai hadi Disemba 2012 ikiwa ni makusanyo halisi kwa kipindi hicho.

Awali bodi hiyo ililenga kukusanya shilingi bilioni 81.846 katika kipindi hicho lakini ilishindwa kufikia makusanyo hayo kutokana na sababu mbalimbali.

Akizungumza na Zanzibar Leo ofisini kwake Mazizini, Kaimu Meneja, Idara ya Usajili na Huduma kwa Walipakodi, Safia Is-hak, alizitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na kupungua kwa idadi ya watalii waliotembelea Zanzibar kutokana na matatizo ya kifedha yaliyoikumba dunia.

Sababu nyengine ni pamoja na kutokusambazwa kwa bidhaa ya mafuta ya nishati katika kiwango kinachokidhi mahitaji jambo ambalo linapelekea kushamiri kwa biashara ya magendo ya mafuta ya nishati.


Sambamba na hayo,alisema sababu ya kutokuanza kukusanywa kwa mapato kutoka katika baadhi ya vianzio vya mapato ya mawizara ni mambo yaliopelekea kutofikia makusanyo yaliyotakiwa.


Hata hivyo,alisema licha ya kutofikia  lengo la makusanyo lililolengwa lakini kwa kipindi hicho cha makusanyo kilionekana kukua ukilinganisha na miezi kama hiyo katika kipindi cha mwaka 2011/2012 ambapo ZRB ilikadiria kukusanya shilingi  59.9 bilioni na kukusanya shilingi 59.6 bilioni sawa na asilimia 99.4 ambapo ni ongezeko la mapato la shilingi  bilioni 8 sawa na asilimia 13.5.

Safia alisema ili kuona kwamba bodi ya mapato inakusanya mapato kama ilivyokusuidiwa ni lazima kuwepo kwa mashirikiano makubwa kati ya wananchi hasa katika suala zima la kudai risiti wakati wa kununua bidhaa mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.