Habari za Punde

19 Wabomolewa Nyumba Kwenye Vianzio vya Maji

Na Khamisuu Abdallah
MAMLAKA ya Maji Zanzibar (ZAWA) imevunja nyumba 19 na msingi 16 katika maeneo ya Mwanyanya na Mtoni baada ya wamiliki wake kujenga katika vianzio vya maji na kukaidi amri ya serikali.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia buldoza likibomoa nyumba moja baada ya nyengine ambazo baadhi yao tayari zilikuwa zimehamiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari,Afisa Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Zahor Suleiman Khatib, alisema operesheni hiyo imekuja baada ya mamlaka kupewa ruhusa na serikali kuvunja nyumba hizo.

Alisema maeneo hayo ni kitovu cha maji na serikali ilizuia kufanyika shughuli zozote za ujenzi wa nyumba za makazi.

“Maeneo haya ni mavuno ya maji na tulipiga marufuku tokea zamani na kuweka mipaka ya nguzo na tuliwafahamisha vizuri wananchi wasijenge kwenye vianzio vyetu vya maji lakini cha kushangaza mipaka yetu wameing’oa na wamejenga nyumba, wanaonesha wazi kuwa wamekaidi amri yetu,”alisema.

Aidha alisema chemchem ya maji ya Mwanyanya imepunguza uzalishaji wa maji kutoka lita bilioni 6.6 kutoka mwaka 1998- 2011 hadi kufikia lita bilioni 1.3, hali inayosababisha wananchi kukosa huduma ya maji.

Hata hivyo, alisema ZAWA itahakikisha inadhibiti vianzio vya maji visiendelee kujengwa makazi ya watu.
Ubomoaji huo ulifanywa chini ya ulinzi mkali wa Polisi,Valantia na KMKM.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.