Habari za Punde

UVCCM wampongeza JK kutimua mawaziri

Na Bashir Nkoromo
UMOJA wa Vijana wa CCM, Kata ya Mabibo, Kinondoni jijini Dar es Salaam, umempongeza Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Jakaya Kikwete kwa kuwavua uongozi mawaziri wanne mwishoni mwa wiki.
Mawaziri waliovuliwa uongozi kufuatia Rais Kikwete kutengua teuzi wao ni, Dk. Emmanuel Nchimbi (Waziri wa Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai (Waziri wa Ulinzi), Mathayo David Mathayo (Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi) na Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii) ambaye ndiye pekee pamoja na uteuzi wake kutenguliwa na Rais lakini alitangaza kujiuzulu akiwa bungeni.
Kutenguliwa kwa uteuzi wa mawaziri hao kulitangazwa rasmi Bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, hatua iliyotokana na mapendekezo ya bunge, baada ya Kamati yake ya kudumu ya  Ardhi, Maliasili na Mazingira kubaini 'uozo' katika operesheni iliyofanyika hivi karibuni ya tokomeza ujangili.
Pongezi hizo ya UVCCM Mabobibo, ni miongoni mwa maazimio waliyofikia wajumbe wa Baraza Kuu la UVCCM kata hiyo, baada ya semina yao iliyomalizika jana na  kufunguwa na Katibu wa Jumuia ya Wazazi mkoa wa Dar es Salaam, Nd. Mohamed Cholage.

Katika maazimio hayo, UVCCM walipongeza ziara za Katibu Mkuu wa CCM, Nd. Abdulrahman Kinana alizofanya hivi karibuni na kumuomba kuendeleza ziara hizo, kwa maelezo kwamba zimeonesha manufaa makubwa kwa chama.
Vijana hao pia wameazimia kuhakikisha mitaa mitatu iliyopo chini ya chama cha CUF, kati ya sita ya kata ya Mabibo inarejeshwa kwenye himaya ya CCM baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika mwakani.Akizungumza katika semina hiyo, Cholage aliunga mkono maazimio hayo, akiyaeleza kwamba ni ya msingi.
"Kwa kweli naunga mkono maazimio. Siyo kwamba tunafurahi mawaziri hawa kukosa kazi, la hasha, lazikini kinachotufurahisha zaidi ni kuona kwamba Mwenyekiti wa chama amesimamia inavyostahili misingi ya uwajibikaji,” alisema.
Aliwahimiza vijana kuwania nafasi za uongozi wa mitaa, uchaguzi utakapowadia, lakini akawataka kufanya hivyo kwa kujipima kwanza kama anatosha kila atakayekuwa anadhamira ya kugombea.
Aliwataka UVCCM kuwa imara katika kukilinda chama akiwakumbusha kuwa wao ndio askari wa mbele katika kazi hiyo.

Aliwaasa vijana kujiepusha na tabia ya kulalamika badala yake wawe mstari wa mbele kukosoa katika njia zinazostahili na kisha kuonesha njia wanazoona zinafaa kutumika katika utatuzi wa changamoto zinazowakabili.

1 comment:

  1. Shamsi Vuai (Waziri wa Ulinzi) nae waziri mzigo? masikini kaka angu kutetea kote muungano kule leo wanasema wewe mzigo? ama hawa hawana shukurani.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.