Habari za Punde

Maalim Seif Ahudhuria Mkutano wa Vyama vya Siasa vya Kiliberali na Democrat

Na Hassan Hamad CAPE TOWN.                                           
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema wakati umefika kwa viongozi wa Afrika kufuata maoni na matakwa ya wananchi, ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima baina ya viongozi na wananchi.

Amesema mara nyingi wananchi huamua kupingana na serikali baada ya kuona haki zao za msingi zinakiukwa, jambo ambalo serikali za sasa zinapaswa kuzingatia madai na haki za wananchi ili kuondosha mivutano hiyo.

Mhe. Maalim Seif ametoa nasaha hizo wakati akizungumza kwenye mkutano wa tisa wa Muungano wa vyama vya Kiliberali na Democrat kwa baadhi ya nchi za Ulaya, Pacific, Afrika na Caribbean (ALDEPAC)unaofanyika mjini Cape town nchini Afrika ya Kusini.

Amesema wananchi wamekuwa wakikabiliwa na matatizo mengi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ambayo wanapoyapeleka serikalini huwa hayazingatiwi, hali inayopelekea kuibua hamasa miongoni mwa wananchi kuanzisha makundi haramu kupingana na serikali.

Mhe. Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema iwapo madai ya wananchi yatasikilizwa na kupatiwa haki zao za msingi hasa zile za kikatiba, pamoja kuzingatiwa kwa tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, mivutano baina ya wananchi na serikali zao inaweza kupungua.

Ametaja matatizo yanayozisumbua nchi nyingi za Afrika kuwa ni pamoja na umasikini, njaa, ukosefu wa ajira na utawala bora.
Amewaambia wajumbe wa mkutano huo kwamba Afrika sio tena bara lenye kiza, bali raia wake wameamka na kudai mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa ili kila raia aweze kuishi katika maisha bora yenye tija.

“Waafrika sasa wanahitaji maendeleo ya kiuchumi, elimu bora, huduma za afya, maji safi na salama pamoja na kuungwa mkono katika miradi yao ya maendeleo”, alifahamisha Maalim Seif na kuongeza,

“Kubwa zaidi wananchi wanataka uwajibikaji na uwazi katika serikali zao, pamoja na kuwepo uhuru wa kutoa maoni na kuheshimiwa kwa haki za binadamu”.

Amemshukuru Rais wa Muungano wa vyama vya Kiliberali Barani Afrika, Olivier Kamitatu, kwa kuamua kufanya mkutano wao mkuu Zanzibar mwezi uliopita, ambao amesema ulikuwa na mafanikio makubwa.

Mhe. Maalim Seif yuko nchini Afrika ya Kusini kwa mwaliko maalum wa muungano wa vyama vya kiliberali kuhudhuria mkutano huo.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.