Habari za Punde

Madiwani wamtimua Mkurugenzi Arusha

Na Joseph Ngilisho,Arusha
BARAZA la Madiwani wa halmashauri ya jiji la Arusha,limemtimua Mkurugenzi wa jiji hilo, Nd. Sipora Liana na wakuu wake wa idara, katika  kikao cha madiwani baada ya kumpigia kura,wakidai Mkurugenzi huyo amezidi kuwadharau na kuwakejeli.
Hali hiyo ilijiri mapema jana wakati madiwani hao walipochachamaa ndani ya kikao wakidai hawawezi kujadili mada yoyote hadi wapate ufafanuzi juu ya dharau wanazodai zinafanywa na Mkurugenzi huyo kwa madiwani.
Naibu Meya, Nd. Prosper Msofe, aliyekuwa akiongoza kikao hicho aliamuru kupigwa kura za kumjadili Mkurugenzi baada ya kutolewa hoja kutoka kwa diwani wa Sekei, Nd. Crisipin Tarimo, kutaka baraza hilo lijigeuze kamati kumjadili Mkurugenzi.
Hoja hiyo ilipokewa na Mwenyekiti wa kikao hicho na aliamuru baraza hilo kujigeuza kamati baada ya nusu ya wajumbe kuunga mkono hoja hiyo ambapo kwa pamoja walimtaka Mkurugenizi na wakuu wake wa idara watoke nje ya ukumbi.Madiwani hao wakiwa kama kamati walianza kumjadili Mkurugeninzi huyo huku kila mmoja akitupa lawama juu yake wakidai wamechoshwa kudharauliwa ikiwemo kutofanyiwa kazi kwa maazimio wanayoyapitisha.

Awali diwani wa viti maalumu kupitia  CCM, Nd. Belinda Kabuje alisema hawataweza kufanya kazi na Mkurugenzi mwenye dharau dhidi ya madiwani na kwamba madiwani palei wanapomfuata ofisini kwa ajili ya kueleza kero zao anawajibu kwa nyodo na dharau kubwa.
“Huyu Mkurugenzi ana dharau sana, ni mwanamke kama mimi lakini amekuwa na dharau utazani si mwanamke ,hatuwezi kukubali kufanya kazi na mtu wa namna hii,” alisema.
Baada ya kamati hiyo kumalizika, Naibu Meya alisema kikao hicho kilikuwa kizito na kwamba makubaliano yaliyotoka katika kamati hiyo ni kwamba madiwani wataandika maoni dhidi ya tuhuma za Mkurugenzi na yatapelekwa kwa mkuu wa mkoa kwa ajili ya kuitisha kikao na kutoa ufafanuzi wa jambo hilo.

Akizungumzia hali hiyo Mkurugenzi, Nd. Sipora Liana aliwashangaa madiwani hao kwa kujigeuza kamati kwa lengo la kumjadili na kueleza kwamba,madiwani hao hawana ubavu wa kumjadili yeye.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.