Na Joseph Ngilisho, ARUSHA
KAMATI ya Bunge ya hesabu za serikali ya mtaa (LAAC), imebaini upotevu
mkubwa wa fedha za maendeleo katika halmashauri ya jiji la Arusha, huku
ikiituhumu kamati ya fedha kushindwa kusimamia fedha zinazotengwa kwa ajili ya
miradi ya wananchi.
Aidha kamati hiyo imemshutumu Meya wa jiji la Arusha, Gaudence Lyimo,
ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya fedha kwa kuhusika na wizi wa mamilioni ya
fedha.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rajab Mohamed, alisema kamati imebaini wizi
wa kutisha kupitia fedha za miradi ya maendeleo ya jamii, ambapo sekta hiyo
hutengewa asilimia 10 ya bajeti ya kila mwaka ya halmashauri hiyo.
Alisema bajeti ya mwaka 2011/12 jumla ya shilingi milioni 391
zilitengwa huku fedha zilizotumika zikionyesha ni shilingi milioni 30 pekee na
fedha nyengine hazijulikani zilipo.
Pia alisema taarifa ya fedha ya mwaka 2012/13 sekta hiyo ilitengewa
shilingi milioni 518 lakini fedha zilizotumika ni shilingi milioni 75, tu huku
fedha nyengine zikiishia matumboni mwa wajanja.
Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walionesha kusikitishwa na ubadhirifu
wa fedha hizo na kumtaka mwanasheria wa jiji hilo, Kiomoni Kibamba awafungulie
mashtaka wahusika.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Ezekiel Maige, alisema baadhi ya
watendaji wamekuwa na tabia ya kukopeshana fedha za miradi, ambapo kwenye
taarifa zao hubainisha kwamba fedha zimekopwa na wananchi na makundi ya vijana
na wanawake.
Naye Mbunge wa Karatu, Israel Natse, alitaka halmashauri hiyo ifutwe
kwani inaongoza kwa hati na matumizi mabaya ya fedha.
Aidha alimtaka Meya wa jiji la Arusha, aeleze kwanini amekuwa
akipitisha fedha za miradi wakati akijua haziendi kwa wananchi.
Kamati hiyo pia ilifichua upotevu wa shilingi milioni 225 fedha ambazo
zilitengwa kwa ajili ya maendeleo ya vijiji lakini zilipitishwa na
hazikuwafikia walengwa ambao ni wenyeviti wa vijiji kwa ajili ya maendeleo ya
vijiji vyao.
Pia kamati imebaini halmashauri hiyo imekuwa ikiidhinisha malipo hewa
kwa wakala pindi anapofikia ukomo wa mkataba.
Akijibu shutuma hizo, Meya Lyimo, alisema hafahamu chochote juu ya
upotevu wa fedha hizo na kuahidi kufuatilia.
Hata hivyo, alisema kuhusu shutuma za jiji kutofikia malengo ya
makusanyo ya ndani inatokana na sababu za kisiasa inayolikumba jiji la Arusha.
No comments:
Post a Comment