Na Mwandishi wetu
NCHI za Afrika zimetakiwa kuwa na msimamo
mmoja kuhusu jinsi ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Misimamo huo wa Afrika unatarajiwa
kuwasilishwa kwenye mkutano mkubwa wa
Dunia kuhusu masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa unaotarajiwa kufanyika New York, Marekani
Septemba, 2014.
Akiwakilisha ripoti ya Kamati ya Viongozi
wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani, katika mkutano wa viongozi wa Afrika (AU), Rais Kikwete alisema kamati
yake inataka kujikita na kujihusisha na masuala
yanayohusu fedha na teknolojia, hatua za kupunguza madhara, na hatua mtambuka ambazo zitahusisha progamu
za vijana, wanawake na hata kuhusisha
Balozi mbali mbali za Afrika katika suala zima la mabadiliko ya hali ya
hewa na pia kuhusisha Jumuiya ya Kimataifa na kufuatilia mapendekezo mbali mbali.
Aliziasa nchi za Afrika kuwa na utashi wa
kisiasa na lengo la pamoja katika kukabiliana na suala hilo ili kufanikisha lengo la dunia la hali ya hewa katika kipindi cha nusu ya pili ya karne
ijayo.
Alisema ili kufanikisha juhudi hizo, bara
la Afrika linahitaji msaada mkubwa wa fedha na teknolojia ya kisasa.
Mapema katika kikao hicho ambacho pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa (UN) ,Ban Ki Moon, Rais Kikwete alisema mkutano ujao wa UN
kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa duniani ni chachu ya makubaliano ya mkataba wa
hali ya hewa ifikapo 2015.
Ripoti za karibuni kuhusu mabadiliko ya hali
ya hewa inaonesha hali ya kilimo, afya, maji na nishati ziko hatarini na kwamba
joto duniani limepanda kwa sentigredi 0.85, hali ambayo inaashiria hali mbaya.
No comments:
Post a Comment