Na Fatina Mathias, Dodoma
Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, amekiri kuwepo tatizo la wizi wa fedha
za Watanzania unaofanywa na kampuni za simu za mikononi, ambazo zinawakata
wateja fedha zao kiholela.
Kauli hiyo aliitoa jana bungeni
mjini hapa alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Konde, Khatibu Said
Haji, aliyetaka kujua ni nani aliyeko nyuma ya pazia huku serikali makini ya
CCM ikikaa kimya bila kuchukua hatua na kuacha mamilioni ya Watanzania
yakiibiwa na kampuni za simu.
Alisema kumekuwepo na tatizo
hilo na kwamba ni kubwa ambapo katika kulidhibiti wameweka kanuni na taratibu
za kudhibiti vitendo hivyo.
“Ni kweli kabisa Watanzania waliko vijijini
ambao ndio wengi hawana uwezo wa kumudu gharama za kusafiri hadi Dar es Salaam
kwenye makao makuu ya kampuni ya simu kwa ajili ya kudai fedha hizo wanazokatwa
na pia serikali ilibaini kuwepo tatizo la kampuni za simu kuwa na utaratibu wa
kupuuza wateja na kuchelewa kufanyia kazi malalamiko ya wateja,”alisema.
Alisema baada ya kulibaini hilo
waliamua kutoa utaratibu wa kawaida wa wateja kulalamika kwenye kampuni za
simu.
“Wateja wamekuwa wakipata shida kwani hata
wapopiga simu kwa ajili ya kulalamika hujikuta wakikatwa tena fedha zao hivyo
kama serikali tunalitambua suala hili,”alisema.
Hata hivyo, alisema wameweka
mtambo maalum wa kufuatilia mawasiliano
ambayo kazi moja wapo ni kufuatilia mapato, kuimarisha huduma za mawasiliano na
kutakuwa na namba za bure ambazo zitasambazwa kwa Watanzania kwa ajili ya
kupiga na kutoa malalamiko yao ambapo kila lalamiko litapewa namba maalumu.
Aidha alikanusha vikali CCM
kuhusika na wizi wa fedha za Watanzania kwa njia ya mitandao unaotokana na kampuni ya simu.
Akijibu swali la msingi,
Makamba alisema Serikali kwa kutambua umuhimu wa kulinda haki za walaji wa
huduma za mawasiliano, mwaka 2011 ilitunga kanuni za kulinda walaji ambazo
zinabainisha haki na wajibu wa watumiaji wa huduma hizo.
Alibainisha pale ambapo
itathibitishwa kwamba kampuni ya simu imekiuka masharti ya mkataba na leseni ya
huduma kwa wateja, kampuni husika hupaswa kumlipa fidia mteja wake.
Aliwaasa watumiaji wa huduma za
mawasiliano wawe wanawasilisha malalamiko katika ngazi husika kama sheria na
kanuni zinavyoagiza.
No comments:
Post a Comment