Rais wa Zanzibar na Mwenyekiri wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Waziri wa Nchi Maendeleo,Biashara na Ushirikiano wa Ireland Bw.Sean Sherlock wakati alipofika Ikulu Mjini Zanzibar akiwa na Ujumbe aliofuatana nao.[Picha na Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiri wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Waziri wa Nchi Maendeleo,Biashara na Ushirikiano wa Ireland Bw.Sean Sherlock wakati alipofika Ikulu Mjini Zanzibar akiwa na Ujumbe aliofuatana nao.[Picha na Ikulu.]
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
19.3.2015
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amefanya mazungumzo na Waziri wa Nchi,
Maendeleo, Biashara na Ushirikiano wa Ireland Mhe. Sean Sherlock na kumueleza
mikakati iliyowekwa na Serikali anayoiongoza katika kuimarisha sekta za
maendeleo sambamba na kusimamia na kuendeleza amani na utulivu uliopo.
Dk. Shein
aliyasema hayo leo huko Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Waziri
wa Nchi, Maendeleo, Biashara na Ushirikiano wa Ireland Mhe. Sean Sherlock akiwa
amefuatana na Balozi wa Ireland nchini Tanzania Mhe. Fionnuala Gilsenan.
Katika maelezo
yake Dk. Shein alimueleza Balozi huyo pamoja na ujumbe aliofuatana nao hatua
mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuhakikisha sekta za maendeleo zinaimarika hapa nchini.
Dk. Shein
alieleza kuwa miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali ni kuhakikisha
inaimarisha Vyuo vyake vya Amali kwa lengo la kutoa mafunzo ya kuwatayarisha
vijana wanaomaliza masomo katika vyuo hivyo kujiajiri wenyewe.
Alisema kuwa
tayari Serikali imeshajenga vyuo vya Amali kwa upande wa Unguja na Pemba na
juhudi zinaendelea kuviimarisha sambamba na azma ya kuviongeza vyengine ili
viweze kukidhi haja ya kutoa mafunzo kwa vijana huku serikali ikijitahidi
katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya masomo vyuoni
humo.
Akieleza kuhusu
sekta ya afya, Dk. Shein alieleza juhudi za makusudi zinazochukuliwa na Serikali
katika kuhakikisha sekta hiyo inaimarika ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vya
akina mama na watoto hatua ambayo inaonesha mafanikio kila kukicha.
Aidha, Dk. Shein
alieleza juhudi za Serikali katika kuhakikisha uchumi wake unazidi kuimarika pamoja
na kupiga hatua katika kutekeleza malengo yake ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na
Kupunguza Umasikini (MKUZA).
Kwa upande wa
Serikali anayoiongoza chini ya muundo wa Umoja wa Kitaifa, Dk. Shein alisema
kuwa Serikali hiyo, inaendelea vizuri na mafanikio makubwa yameweza kupatikana
tokea kuanzishwa kwake hadi hii leo.
Alisisitiza kwamba
kubwa kuliko yote ni kuhakikisha amani na utulivu inaendelea kuwepo hapa nchini
kwa wakati wote huku akisisitiza hatua hiyo kuendelezwa na kusimamiwa na
Serikali anayoiongoza hasa katika wakati huu wa kuelekea upigaji kura za maoni
juu ya Katiba inayoopendekezwa sambamba na uchaguzi mkuu ujao.
Katika hatua za
kuendeleza amani na utulivu hapa nchini, Pia, Dk. Shein alimueleza Balozi Sherlock
juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha suala zima la ulinzi na
usalama kwa ajili ya watalii linaimarishwa ili kuufanya utalii wa Zanzibar
uzidi kupata sifa na kuwa kivutio kwa watalii kutoka kila pembe ya dunia.
Aidha, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kutoa pongezi zake kwa Ireland kwa kuendeleza ushirikiano
na uhusiano kati yake na Zanzibar na kusisitiza haja ya kuimarishwa zaidi ushirikiano
huo ili kuleta manufaa kwa pande zote mbili.
Dk. Shein alieleza
haja ya kuendeleza ushirikiano katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo
sekta ya kilimo na sekta nyenginezo huku akitoa pongezi zake kwa nchi hiyo kwa
kuiunga mkono Zanzibar katika kusaidia katika sekta ya afya, miundombinu na
mawasiliano, huduma za zimamoto, ufugaji na sekta nyenginezo.
Nae Waziri wa
Nchi, Maendeleo, Biashara na Ushirikiano wa Ireland Mhe. Sean Sherlock alimueleza
Dk. Shein kuwa Ireland inathamini sana uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar
hasa kwa kutambua kuwa Ireland na Zanzibar zote ni visiwa.
Waziri Sherlock
alisema kuwa Ireland itaendelea kutoa ushirikiano wake na kuendelea kuiunga
mkono Zanzibar katika uimarishaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo huku
akiahidi Serikali yake kuunga mkono uimarishaji wa Vyuo vya Amali hapa
Zanzibar.
Alisema kuwa
tokea mwaka 1979 Ireland imekuwa na mahusiano mema na Tanzania ikiwemo Zanzibar
hatua ambayo inaendelezwa hadi hivi leo.
Aidha, Waziri
Sherlock alieleza kuwa mafanikio yaliofikiwa hapa nchini katika kuimarisha
sekta za maendeleo ni ya kupigiwa mfano na kuna kila sababu ya kuendelea
kuyaunga mkono. Waziri huyo alieleza
azma ya Serikali yake ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano na Zanzibar
hasa katika maeneo mapya ya kimaendeleo.
Mnamo mwezi
Disemba mwaka jana Wabunge wa Bunge la Ireland walitembelea Zanzibar na kufanya
mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindyuzi Dk. Ali
Mohamed Shein ambapo katika mazungumzo hayo suala la kuimarisha uhusiano na
ushirikiano baina ya opande mbili hizo lilisisitizwa.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment