Habari za Punde

Ugonjwa wa Homa ya Typhoid wazuka Mkoa mjini wa Magharibi

Kutokana na taarifa iliyotolewa na Wizara ya afya Zanzibar ni kwamba kuna ugonjwa wa homa ya taifodi (typhoid fever) umejitokeza Mkoa wa Mjini Magharibi.
 
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ugonjwa huo unaenezwa na Bacteria anaejulikana kwa jina la Salmonella Typhi, na maambukizi ya ugonjwa huo hayawezi kutoka kwa mnyama kwenda kwa binadamu bali huambukizwa kutoka kwa binadamu mmoja kwenda mwengine.
 
Aidha taarifa hiyo imeelezea kuwa dalili za ugonjwa huo kama zifuatazo; Homa kali, Mwili kulegea, Kuumwa na tumbo, Kukosa choo, Kuumwa kichwa, Kuharisha na Kutapika, Kufanya vipele mwilini vyenye rangi ya wardi (Rose) na hatimae ugonjwa huo ukiwa mkali mgonjwa anaweza kuchanganyikiwa.
 
Taarifa hiyo imetanabahisha kuwa ugonjwa huo huenezwa kwa njia ya Kula au Kunywa chakula au maji yenye vimelea vya ugonjwa huo, Kupitia katika kinyesi au haja ndogo ya mtu mwenye maambukizi ya homa hiyo ambapo Nzi anaweza kuhamisha Bakteria kutoka katika kinyesi na kupeleka katika chakula au maji, pamoja na kutokunywa maji bila ya kuchemsha na kula chakula ambacho kimewekwa wazi au kisichokuwa cha moto.
 
Taarifa hiyo imefahamisha juu ya kujikinga na ugonjwa huo, ikiwemo kuweka usafi majumbani, kufunika chakula ili kuepuka nzi, kuosha mikono kabla na baada ya kula kwa kutumia maji ya kutiririka na sabuni wakati wa kuandaa chakula.
 
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ugonjwa huo unaweza kupimwa kwa vipimo vya maabara kwa njia ya kupimwa Damu, Kinyesi na Damu ndani ya mifupa.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa hadi sasa wagonjwa 16 wanaripotiwa kupatikana kupitia hospitali kuu ya Mnazi Mmoja ambapo kati ya hao 6 ni wanawake, 10 ni wanaume, na katika wagonjwa hao chini ya miaka 5 ni 4 na juu ya miaka 5 ni 12.
 
Maeneo yanayoripotiwa kupatikana kwa wagonjwa hao ni kama yafutayo;
Mtopepo =3
Mwera =1
Mwembeladu=2
Mbuyuni=1
Kwa Mtipura=1
Tomondo=3
Mwembetanga=1
Kibweni=1
Chumbuni=1
Kinuni=1
Nyarugusu=1
 
 
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.