Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dk Shein, Azungumza na Balozi wa India Ikulu Zanzibar.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                                                                             10.9.2015
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa India  na Zanzibar zina uhusiano na ushirikiano wa kihistoria hivyo hatua za nchi hiyo za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar zimeweza kuleta manufaa kwa pande zote mbili.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati wa mazungumzo kati yake na Balozi mpya wa  India katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Sandeep Arya, aliefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha.

Katika mazungumzo hayo, Dk.Shein alisema kuwa Tanzania ikiwemo Zanzibar zina uhusiano na ushirikiano wa kihistoria na India ambao umeanzishwa na  waasisi wa nchi hizo akiwemo marehemu Julius Kambarage Nyerere na marehemu Mzee Abeid Amani Karume  kwa mashirikiano na waasisi wa nchi hiyo akiwemo marehemu Indira Gandhi.

Akielezea juu ya ushirikiano na uhusiano kati ya India na Zanzibar, Dk. Shein alimueleza Balozi Arya kuwa Zanzibar inathamini sana ushirikiano uliopo hatua ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ushirikiano katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo elimu, afya, biashara, miundombinu, huduma za kijamii na nyenginezo.

Kwa upande wa  ushirikiano uliopo katika sekta ya elimu, Dk. Shein aliipongeza India kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi kadhaa za masomo kwa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuwapatia nafasi hizo watendaji wa Serikali kwa lengo la kuongeza ufanisi na kusisitiza haja ya kuongezwa kwa nafasi hizo.

Pia, alipongeza hatua za mashirikiano zilizofanyika kati ya Zanzibar na India katika uanzishwaji wa Chuo cha amali cha “Barefoot college” katika kijiji cha Kinyasini Mkoa wa Kaskazini Unguja ambacho alikizindua hivi karibuni ikiwa ni matunda ya ziara yake aliyoifanya nchini India  Februari mwaka 2014.


Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumueleza Balozi Arya, mafanikio yaliofikiwa hapa Zanzibar katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya utalii hatua ambayo imepelekea kufungua afisi nchini humo katika mji wa Mumbai. Pia, alimueleza kuimarika kwa  mahusiano kati ya wananchi wa India na Zanzibar yaliopelekea kukuza ushirikiano wa kijamii na kiutamaduni.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliendelea kuipongeza India kwa kuendeleza ushirikiano wake na kuunga mkono miradi ya maji, elimu na mengineyo huku akipongeza hatua zinazoendelea za kutekeleza makubaliano yaliofika katika ziara yake nchini India.

Nae Balozi mpya wa India katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Sandeep Arya  alipongeza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya India na Zanzibar na kuadi kuuendeleza.

Balozi Arya alisema kuwa India itahakikisha inakamilisha miradi yote ya maendeleo ilioanzishwa kwa mashirikiano kati yake na Zanzibar sambamba na kuongeza nafasi za masomo kwa Zanzibar huku akiahidi juhudi maalum zitaendelea kuchukuliwa katika kuutangaza utalii wa Zanzibar nchini India.

Aidha, Balozi Arya, alisema kuwa juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha sekta ya uwekezaji na biashara zinaimarika kati ya nchi mbili hizo sambamba na kuongeza nafasi za masomo nchini humo.

Wakati huo huo, Dk. Shein alifanya mazungumzo na Mhe. Hemed Idd Mgaza, Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Saud Arabia aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kusalimia na kuaga rasmi.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi Mgaza kuwa Tanzania imekuwa na uhusiano mwema na Saud Arabia ambapo nchi hiyo imeweza kutoa misaada kadhaa ya kuendeleza sekta za maendeleo na ni nchi yenye mahusiano makubwa na nchi nyengine duniani hivyo ipo haja ya kukuza uhusiano na ushirikiano uliopo.

Kwa upande wa Zanzibar, Dk. Shein alisema Saud Arabia imeweza kusaidia sekta ya elimu na kutolea mfano Chuo Kikuu cha mwanzo cha Zanzibar kiliopo Tunguu ambacho kimejengwa na Darul Imaan kutoka Saudia, miundombinu zikiwemo barabara za Kaskazini Pemba ambazo amezizindua hivi karibuni zenye km 35 ikiwemo Wete-Konde na Wete-Gando, sekta ya maji, umeme na nyenginezo.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa hivi sasa Tanzania imekuwa ikichukua juhudi za makususdi katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa uchumi wa kidiplomasia na nchi rafiki duniani hivyo, ipo haja kwa Tanzania kukuza uhusiano wake na Saudia katika nyanja hiyo.

Nae Balozi Magaza, alimueleza Dk. Shein shukurani zake kwa viongozi wa kitaifa kwa uteuzi wake huo huku akiahidi kutekeleza kazi zake kwa ufanisi na mashirikiano makubwa kwa lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Saud Arabia.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.