Habari za Punde

Wananchi watimiza haki yao ya kidemkrasia kwa kupiga kura leo

Na Othman Khamis Ame, OMPR

Hatimae ile siku ya Jumapili ya Tarehe 25 Oktoba  ambayo Watanzania walikuwa wakiisubiri kutoa maamuzi ya  kutumbukiza kura ili kukipa dhamana chama kilichonadi  vyema sera na Ilani yake na kukubalika imetimia.

Watanzania hao wamepata fursa ya kutimiza haki yao ya kidemokrasia ya kuwachagua viongozi watakaowaongoza katika kipindi cha miaka mitano  ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa ulioanza mwaka 1995 takriban chaguzi Tano sasa.

Wapiga kura wa upande wa Tanzania Bara  waliokuwa chini ya usimamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi { NEC } wamewajibika kupiga kura  kwa nafasi Tatu za Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Ubunge na Udiwani wakati wale wa Zanzibar wamepiga kura kwa nafasi  Tano za Urais wa Muungano, Ubunge,Urais wa Zanzibar,Uwakilishi pamoja na Udiwani.

Moja kati ya jambo lililoleta faraja ndani ya vituo vya wapiga kura  Mjini na Vijijini ni ile hali ya amani na usalama iliyotanda ambayo ilikuwa ikisisitizwa kulindwa na kudumishwa wakati wa Kampeni za uchaguzi zilizochukuwa takriban mwezi mmoja.

Viongozi mbali mbali pamoja na maelfu ya wananchi walijitokeza mapema asubuhu kupiga kura na kutimiza ile kiu yao iliyowashika tokea kuanza kwa zoezi ya kura za maoni, uandikishaji wa daftari la wapiga kura, kampeni hadi upigaji kura wenyewe.

Misururu mirefu ya Wananchi  iliyowekwa kwa mujbu wa mfumo wa majina ya wapiga kura ilianza mapema alfajiri  mara tuu baada ya wale wananchi waumini wa dini ya Kiislamu kutoka misikitini kutekeleza Ibada ya sala ya Asubuhi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Sheni na Mkewe Mama Mwanamwema Shein walipiga kura katika Kituo chao cha kupiga kura cha Kijiji cha Kibele Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi wakapiga kura katika Kituo chao kiliopo Skuli ya Sekondari ya Kitope Jimbo la Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja saa 2.25  za asubuhi.

Balozi Seif  pia ni mgombea wa nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi katika Jimbo hilo jipya la Mahonda kwa mujibu wa mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar kufuatia ongezeko na idadi ya watu kwa mujibu wa Sensa ya Idadi ya watu na Makaazi ya mwaka 2012.

Akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kupiga kura Balozi Seif  alisema ameridhika na zoezi zima liloanza mapema asubuhi ambapo wananchi mbali mbali tayari wameshatumia haki yao ya kupiga kura na kurejea nyumbani kuendelea na shughuli zao za kimaisha.

Balozi Seif aliwaomba wananchi kuepuka kukaa vituoni kwa ushawishi wa kutaka kulinda kura kwani ni vyema suala hilo likaachiliwa Mahkama kutoa uamuzi kwa vile tayari liko mahakamani.

Akigusia suala la mawakala wa vyama Balozi Seif akiwa mgombea wa nafasi ya Uwakilishi jimbo la Mahonda  aliwaomba wagombea wenzake wakazingatia sheria na kanuni za Tume ya Uchaguzi ya kuweka mawaka wanaoishi katika maeneo ya kupiga kura ili kusimamia kura zao.

Alisema kitendo cha baadhi ya wagombea hao kuweka mawaka wanaoishi nje ya vituo vyao vya kupiga kura mbali ya kwenda kinyume na sheria ya Tume ya chaguzi lakini pia kinaweza kuleta vurugu zisizo na msingi wowote.

“ Makawala wanaosimamia wagombea wa uchaguzi lazima wanatakiwa wawe wakaazi wa eneo la kupigia kura kwa mujibu wa sheria na kanuni za Tume ya Uchaguzi “. Alisema Balozi Seif.

Moja kati ya jambo lililoleta faraja kubwa ndani ya zoezi zima la upigaku kura ni ile hali ya amani miongoni mwa wapiga kura katika vituo mbali mbali vya wapiga kura Mjini na Vijijini.

Mmoja kati ya wapiga kura katika kituo cha kupiga kura cha Skuli ya Sekondari ya Kitope ambae alikataa kutaja jina lake alisema ameridhika na maandalizi mazima yaliyofanywa na Tume za Uchaguzi za Taifa na Ile ya Zanzibar na kuwapa fursa wananchi kutekeleza haki yao katika misingi ya utulivu na bila ya usumbufu.

Alisema yule mwananchi atakayefikia maamuzi ya kutaka kuzilaumu Tume za Uchaguzi ajijue kwamba ana matatizo kwa vile fursa ilitolewa mapema kwa wananchi kuangalia majina yao kwa karibu siku nne kabla ya uchaguzi na akapewa nafasi  ya kutoa taarifa ili afanyiwe marekebisho endapo jina lake hakuliona.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.