Habari za Punde

Umoja wa Mataifa Wajadili Tatizo la Dawa za Kulevya.

Pichani ni baadhi ya aina ya dawa za kulevya ambazo,  Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa linajadili katika Mkutano wa Maalum ulioanza  jana  jumanne hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. Mkutano huu unajadili mafanikio, changamoto na nini kifanyike zaidi   katika udhibiti   wa usambazaji, matumizi na  tiba kwa waathirika wa dawa hizo ambazo zimeelezwa kuwa chanzo  cha  kuenea kwa magonjwa mbalimbali  yakiwamo ya  Ukimwi lakini pia faida itokanayo na biashara hiyo kutumika katika kufadhili ugaidi,  rushwa, na kudhoofisha Taasisi za Serikali  zikwamo za Kisheria

Na MwandishiMaalum,  New York
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  jana ( Jumanne) limeanza mkutano wa siku tatu ambao nchi wanachama wanapata fursa ya kutathmini mafanikio,  mapungufu na changamoto ambazo serikali zinakabiliana nazo katika kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya.

Akifungua mkutano huo maalum (UNGASS), Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Bw. Jan Eliason,amesema, dawa za kulevya ni tatizo linaloathiri kila nchi na sekta zote za jamii duniani kote.

Akaongeza kwa kusema,mitandao ya wasafirishaji wa dawa za kulevya inachochea machafuko, rushwa na kudhoofisha taasisi za serikali na utawala wa sheria.

Ujumbe wa  Tanzania katika Mkutano huu maalum,  unaongozwa na Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.

Naibu Katibu Mkuu, akasema hata Baraza la Usalama la Umoja wa Mataia, limethibitisha kuwa faida itokanayo na biashara ya dawa za kulevya inatumika kufadhili ugaidi na siasa za misimamo mikali katika dunia ya leo.

Licha ya faida ya biashara ya dawa hizo kufadhili ugaidi na mtukio mengine ya kihalifu, kwa upande wa watumiaji,  dawa hizo zimesababisha kupotea kwa maisha ya mamilioni ya watu , kuzitia hasara za kiuchumi familia zao na jamii kwa ujumla na pia  zimekuwa ni moja ya chanzo cha kuenea kwa ukimwi,  kifua kikuu na hepatitis.

Hata hivyo amebainisha kuwa,umaskini na kukosekana kwa usawa kunazifanya baadhi ya jamii kujihusisha na uzalishaji na matumizi ya dawa za kulevya.

Akizungumzia huduma kwa waathirika wa dawa za kulevya,  Bw. Jan  Eliason amesema, sera na sheria za kuthibiti dawa za kulevya nyingi zinakwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu kiasi cha kuwafanya waathirika wengi kushindwa kutafuta huduma za tiba na mahitaji mengine ama,kuogopa kuadhibi wa au kulazimishwa kwenda kwenye tiba.

“Nivema basi”, anasema Naibu Katibu Mkuu,“ tukawa na ushirikiano kutoka ngazi za juu katika kuwapatia tiba waathirika, na kutojitafutia faida kutoka kwa waathirika”

Akasisisitiza kwamba jukumu la msingi la mikataba ya kimataifa ya udhibiti wa dawa za kulevya ni pamoja na,kuhakikisha afya na ustawi wa mwanadamu.

Na kwamba, katika matumizi ya mikataba hiyo lazima kuhakikisha uwiano baina ya usalama na usalama wa jamii kwa kuzingatia afya,  haki za binadamu na maendeleo.

Akasema anatambua pia kuwa baadhi ya vipengele vya ajenda ya mkutano huo ni nyeti na tata. “tunafahamu pia  kuwa kuna baadhi ya nchi na kanda ambazo zimeathirika zaidi kuliko nyingine.

Ni  muhimu basi kila mmoja wetu akamsikiliza mwenzie na kujifunza uzoefu wa mtu mwingine.
Amesisitiza kuwa changamoto za kukabiliana na madawa ya kulevya zinahitaji mwitikio , mwendelezo na ushirikiano wa serikali zote,  sekta zote, jamii nzima na Taasisi zote za Umoja wa Mataifa.

Katika siku ya kwanza na UNGASS, nchi wanachama wamepitisha mfumo mpya wa kupambana na kudhibiti dawa za kulevya. 

Mfumo huo umeandaliwa na Tume ya Dawa za Kulevya(CND)na kujadiliwa na nchi wanachama. 

Mfumo huo mpya unatambua na kusisitiza kwamba katika kushughulikia tatizo la dawa za kulevya msisitizo lazima uelekezwe kwa mwathirika,  familia zao, jumuiya na jamii katika ujumla wake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.