STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 20 Mei, 2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Balozi za
Tanzania nchi za nje zinapaswa kuongeza kasi ya
utekelezji wa sera ya diplomasia ya kiuchumi ili
Tanzania izidi kuendelea kuimarisha uchumi wake.
Dk. Shein alimueleza Balozi mpya wa Tanzania nchini
Uingereza Mheshimiwa Asha-Rose Migiro ambaye
alifika ofisi kwake Ikulu kumuaga kuwa Balozi za
Tanzania nchi za nje zimekuwa zikifanya kazi nzuri
kuitangaza Tanzania na hivyo kuchangia katika
kuimarisha uchumi na biashara ikiwemo ya utalii
nchini.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema
uhusiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Uingereza una historia kubwa na ni wenye
mafanikio ya kuridhisha kwa pande zote.
“urafiki wetu na Uingereza una historia ndefu na ndio
umetuweka katika familia moja ya nchi za Jumuiya ya
Madola hivyo kuuendeleza na kuuimarisha ni wajibu
wetu” alisema Dk. Shein.
Alifafanua kuwa nchi hiyo ina ushawishi mkubwa
ulimwenguni hivyo kuendelea kuwa rafiki wa nchi
yetu ni jambo la kujivunia na la umuhimu mkubwa
ambalo tunapaswa kulienzi.
Rais wa Zanzibar alimwambia Balozi Migiro kuwa kwa
mwaka jana Uingereza ilikuwa nchi ya tatu kwa idadi
kubwa ya watalii walioitembelea Zanzibar hivyo nchi
muhimu katika biashara ya utalii kwa Tanzania.
“watalii wakifika Zanzibar wanamaliza shughuli zao
katika mbuga za wanyama Tanzania Bara
halikadhalika kwa watalii wanaoanza safari zao
mbugani Tanzania Bara wengi humalizia Zanzibar”
Dk.Shein alisema na kubainisha kuwa sekta hiyo ni
muhimu kwa uchumi wa Zanzibar na Tanzania Bara
pia.
Alifafanua kuwa sekta ya utalii hivi sasa inachangia
asilimia 27 ya pato la taifa la Zanzibar huku sekta
hiyo ikichangia asilimia 80 ya fedha za kigeni.
Aidha alisema kuimarika kwa sekta hiyo inatokana na
jitihada mbalimbali zikiwemo za balozi za Tanzania
nchi za nje kuitangaza Zanzibar na kuongeza kuwa
Zanzibar hivi sasa inapokea wastani wa watalii
300,000 kwa mwaka kutoka watalii 170,000 mwaka
2010.
Kwa mwelekeo huo, Dk Shein alibainisha kuwa
Zanzibar inatarajia kulifikia lengo la kupokea watalii
500,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2020 kama dira
ya Zanzibar ya 2020 inavyoelekeza.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Balozi
Migiro kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais John
Pombe Magufuli kushika wadhifa huo ambao alieleza
kuwa ni heshima kubwa na kwa mtu mwenye uwezo
kama yeye Dk Migiro.
“Nilipokea kwa furaha uteuzi wako kwa sababu ya
utendaji wako ambao wakati wote umekuwa wa
mafanikio” Dk. Shein alimueleza Balozi Migiro.
Kwa upande wake Balozi Asha-
Rose Migiro aliishukuru serikali na uongozi wa
serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
kuendelea kumuamini kwa kumkabidhi majukumu
hayo muhimu.
“Ahsante kwa Serikali na viongozi wangu kwa
kuendelea kuniamini na kunipa heshima hii kubwa
kuiwakilisha nchi yetu nje”Balozi Migiro alieleza.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
No comments:
Post a Comment