Rais wa Shirika Lisilo la Kiserekali la SHINA INC Bi Jessica Kamala Mushala, akizungumza na wanawake wa Wilaya ya Kusini Unguja baada ya kumaliza mafunzo yao ya kuweza kuibua miradi kumkomboa mwanamke na mtoto katika kupata kipato, wakati wa hafla ya kukabidhi Vyeti kwa Wanavikundi hivyo Vinne vya Shehia ya Nganani Makunduchi.
Rais wa Jumuiya ya SHINA INC Tanzania, Jesica Kamala, ametowa wito kwa akinamama
nchini kushirikiana na kuimarisha huduma za ulezi kwa watoto, ili waweze kuwa
na maisha bora na kupiga hatua ya kielimu.
Rais
huyo ametowa changamoto hiyo leo katika hafla ya kukabidhi vyeti kwa vikundi
vya ujasiriamali vya shehiya ya Kijini, iliofanyika katika ukumbi wa skuli ya
Sekondari Makunduchi.
Jumla
ya wanachama 40 kutoka vikundi vya ‘Mkorofi sio mwenzetu’, ‘Siri Moyoni
mwako’, ‘Dhulma sio njema’ na ‘Manufaa yetu’, wamepatiwa vyeti baada ya kumaliza
masomo ya miezi mitatu kuhusiana na uendeleezaji wa kilimo cha mboga mboga pamoja
na uanzishaji wa biashara ndogo ndogo.
Akizungumza
na wanachama hao, Kamala alisema kuna haja kwa akinababa kutoa nafasi na kuwawezesha
akinamama ili waweze kuwa wazalishaji na kujiendeleza kimaisha.
Alisema
sio lengo la mradi huo kubadilisha tamaduni za asili za wananchi, bali una azma
ya kuwawezesha akinamama kiuchumi, na kuondokana na umasikini.
Aliwataka
akinamama hao kila mmoja kutoa mchango kwa mwenzake kwa kile anachokifahamu,
ili waweze kupiga hatua za kimaendeleo
kwa pamoja.
Aidha
aliahidi kuzichukuwa changamoto zinazowakabili na kuwaomba ndugu na marafiki
nchini Marekani kusaidia katika kuzipatia ufumbuzi wake.
Mapema
katika risala ya wanachama wa vikundi hivyo, iliyosomwa na mwanafunzi Rukia
Abdalla, wajasiriamali hao walisema pamoja na mafanikio waliyofikia,
wanakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo uhaba wa vifaa vya kufanyia kazi na
uelewa duni kwa wanachama wake.
Wamesema
katika uendeshaji wa vikundi vyao, wanakabiliwa na na mahitaji makubwa, huku
uwezo wao kifedha ukiwa duni.
Hata
hivyo risala hiyo imebainisha kuwa vikundi hivyo tayari vimefanikiwa kuzalisha
bidhaa mbali mbali zenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 1.6, ndani ya
kipindi cha 2016.
Aidha
wameiomba Serikali kuunga mkono na kusaidia shughuli za wajasiriamali hao ili
waweze kupiga hatua na kujikwamua katika lindi la umasikini.
Mmoja
wa wajasiriamali waliokabidhiwa vyeti hivyo, Vatima Ali, alisema kutokana na
mafunzo aliyopata, ameweza kujenga uwezo mkubwa katika uendeshaji wa biashara
pamoja na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za kilimo.
Alisema
hivi sasa anaweza kujiendesha na kumudu kugharamia mambo kadhaa, ambapo kabla
ya mafunzo hayo alishindwa kuyamudu.
Jumuiya
ya SHINA INC mbali na kujishughulisha na utoaji wa vifaa na misaada mbali mbali
ya kijamii, kwa wajane, yatima na watoto/watu wanaoishi katika mazingira
magumu, pia hujihusisha na kuwawezesha akinamama katika kuendeleza miradi
midogo midogo ya kilimo na biashara, kwa lengo la kujikwamua katika umasikini.
Katika
hafla hiyo, mbali na wanachama wote wa vikundi hivyo kupatiwa vyeti, pia
walipatiwa mablanket maalum ya kujikinga na wadudu wanaofyonza damu ya
binadamu, ikiwemo mbu, kwa lengo la kujikinga na malaria.
No comments:
Post a Comment