Habari za Punde

Wananchi Watakiwa Kutoa Taarifa Wanapobaini Matukio Yasio ya Kawaida Kwa Jamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Manunuzi na Uondoaji wa Mali za Serikali Zanzibar.Ndg.Othman Juma Othman akizungumza kuhusu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo.

Na.Takdir Ali, Maelezo Zanzibar.
Wakati umefika kwa Wananchi wa Zanzibar kutoa taarifa wakati wanapobaini matukio yasiokuwa ya kawaida kwa wanajamii hasa wafanyakazi wa kada ya manunuzi ili kuweza kubaini namna walivyozimiliki.
Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Mazizini, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Manunuzi na Uondoaji wa Mali za Serikali Othman Juma Othman alisema kuna baadhi ya watendaji wanafanyakazi kwa muda mfupi na kumiliki mali nyingi ambazo zinakuwa vigumu kuzitolea ufafanuzi.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona Mfanyakazi anapoajiriwa katika kitengo cha Manunuzi anamiliki utajiri wa mali ya zaidi ya wafanyakazi 80 na kuwapa wasiwawasi Wananchi.
Alisema Serikali inatumia kiasi ya asilimia 70 ya Fedha katika Bajeti kwa kutoa Zabuni na ununuaji wa Dawa, Ujenzi, Barabara, Viwanja vya ndege, Bandari, Miondombinu ya Maji na Umeme hivyo ni lazima sheria No 11 ya mwaka 2016 imeweka miongozo madhubuti ya kuzuia kufanyika kwa vitendo vya Ubadhirifu.
Amekemea tabia iliojengeka kwa baadhi ya Vijana kutaka kujitajirisha kwa njia ya mkato wakati ni kinyume cha sheria na desturi za wafanyakazi wa zamani waliokuwa wakifanya kazi kwa Uzalendo na Uwajibikaji wa hali ya juu bila kujali maslahi yao binafsi.
“Wazee wetu walikuwa wanafanya kazi hadi kufika kustafu hawakuwa na hata kibanda na pesa zilikuwepo za kutosha ila walitosheka na Mishahara yao,” Alieleza Mkurugenzi Othman.
Aliwaeleza wananchi kuona Bajeti ya Serikali imewekwa kwa ajili ya Maendeleo yao na Mamlaka imeundwa kwa lengo la kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na sio kuingia mifukoni mwa wajanja wachache kwa manufaa yao hivyo amewataka kutoa mashirikiano kwa Mamlaka hiyo.
Alifahamisha kuwa Rushwa kubwa hivi sasa ipo katika masuala ya manunuzi na uagiziaji wa bidhaa na hapo ndipo panapotokea upotevu mkubwa wa fedha na Mamlaka peke yake  bila kushirikiana na raia wema haiwezi kuwagundua wafanyakazi wanaoendesha vitendo vya wizi wa mali za serikali.
Amewataka wafanyakazi wanaoajiriwa katika vitengo vya fedha na manunuzi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa waangalifu na Mamlaka ya Ununuzi na Uondoaji wa Mali za Serikali haitakuwa na muhali kwa wafanyakazi wanaoendesha vitendo hivyo katika taasisi za Serikali.
                Imetowa na Idara ya Habari Melezo Zanzibar.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.