Habari za Punde

Taarifa ya Hali ya Mafuta Zanzibar

Na Mwashungi Tahir       Maelezo. 29-10-2018.
Mamlaka ya udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) imewajuilisha wananchi kuhusu Meli ya MT East Wind inayotumiwa na kampuni ya Zanzibar Petrolium Limited (ZP) imewasili nchini ikiwa na Tani 900 sawa na lita 1,695,632. Ambapo taratibu za mafuta kusambazwa kwenye vituo tayari zimeanza kufanyika .
Akitoa taarifa  kuhusu hali ya mafuta  Zanzibar kwa waandishi wa habari huko kwenye ofisi zao ziliopo maisara Mkurugenzi Mkuu  ( ZURA) Haji Kali Haji akitoa ufafanuzi alisema hali halisi ya uwepo wa mafuta hapa nchini kuanzia Jumapili tarehe 28-10-2018 inaonyesha kwamba upande wa kisiwa cha Unguja kutakuwa na mafuta ya Petroli lita 1,295,632 yanayoweza kutumika kwa muda wa siku 7.
Mafuta ya dizeli lita 2,047,914 yanayoweza kutumika kwa muda wa siku kumi na tatu  na Mafuta ya Taa lita 362,517 yanayoweza kutumika kwa muda wa siku saba 7 .
Aidha alisema   meli hiyo baada ya kushusha mafuta inategemea kupeleka mafuta Pemba ambapo mafuta ya Petrol lita 400,000 yanayoweza kutumika kwa muda wa siku kumi na moja (11) , Mafuta ya Dizeli lita 250, 000 yanayoweza kutumika kweam muda wa siku kumi na moja (11).
Alieleza kuwa meli hiyo inatarajiwa kurudi tena katika Bandari ya Mombasa kupakia Tani 1500 sawa na lita 2,000,000 za Mafuta ya Petroli itawasili trehe 04/11/2018.
Alisema ZURA  imesikitishwa na hali ya uhaba wa mafuta uliojitokeza ambayo imewasababishia wananchi kukosa huduma kikawaida , kutokana na hali hiyo ZURA  inayaagiza Makampuni ya Mafuta kuhakikisha ya kwamba yanasambaza mafuta kwa haraka na kurejesha huduma hiyo kwa wananchi na kuhakikisha inapatikana  bila ya usumbufu.
Pia ZURA inawaomba radhi wananchi kwa usumbufu uliojitokeza na kueleza kwamba inafuatilia kwa karibu matengenezo ya Meli mbili zilizoharibika ili kuhakikisha hali ya upatikanaji wa mafuta nchini inarejea kama kawaida.
Vile vile Mamlaka inawasisitiza wananchi kutosikiliza taarifa zisizo rasmi ambazo zinazopelekea taharuki, matarajio ya ZURA ni kuwa hali ya upatikanaji wa Mafuta Zanzibar itaendelea kuwa nzuri ZURA  pia inawashukuru wananchi kwa kuwa wastahamilivu na kuomba kuendelea kutoa ushirikiano ili kuimarisha huduma ya nishati.
Mwisho
Imetolewa na Idara ya Habari maelezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.